Hiyo ni yao tabia, walevi wakishalewa,
Na wewe watakwambia, ni mlevi umelewa,
Wewe changamkia, na lako ukalistua,
Walevi wakishalewa, husema na wewe mlevi !
Madaraka wakilewa, ndiyo yanayotokea,
Wengine wakishalewa, hayo watawaambia,
Enendeni kutumia, changamoto 'kitokea,
Walevi wakishalewa, husema na wewe mlevi !
Fursa ikitokea, chupa haujanywea,
Wakati umetimia, ya kwako kujifanyia,
Hapo ukishaingia, hutoacha kuchukua,
Walevi wakishalewa, husema na wewe mlevi !
Chenga utajipigia, mwanzo hadi kuishia,
Yako kujikusanyia, na njia kufaragua,
Porini hautakuwa, angani utajapaa,
Walevi wakishalewa, husema na wewe mlevi !
Chini ukajionea, ni wapi pa kushukia,
Ndege ukailengea, kiwanjani kushukia,
Kitu huwezi kosea, shabaha ukiijua,
Walevi wakishalewa, husema na wewe mlevi !
Saturday, December 29, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment