Wednesday, December 5, 2012

D E N I



Deni hili hudaiwa, siku ya kuahidiwa,

Pasina kulitambua, kitanzi unajitia,

Kijana unatakiwa, muda wako kuujua,

Deni hili walijua, utakuja kudaiwa ?

 

Utakuja kuhojiwa, vipi uliutumia,

Ujana uliopewa, katika hii dunia,

Hesabu kuhesabiwa, kwa dakika na masaa,

Deni hili walijua, utakuja kudaiwa ?

 

Kipi ulijipangia, ya kwako kujifanyia,

Kisha ukaachia, ya Mola yaliyokuwa,

Na viumbe kuwafaa, waliowakikuttegemea,

Deni hili walijua, utakuja kudaiwa ?

 

Umri utatakiwa, na huo kuelezea,

Miaka uliyopewa, vipi uliitumia,

Uliifaa dunia, au ulijikusanyia?

Deni hili walijua, utakuja kudaiwa ?

 

Elimu huuliziwa, vipi uliitumia,

Baada kujipatia, nani iliyemfaa,

Ya dini na ya dunia, kiasi kuhesabiwa,

Deni hili walijua, utakuja kudaiwa ?

 

Kama uliizuia, kichwani ikabakia,

Haikuwa manufaa, kwa watu kusaidia,

Nakisi utaambiwa, makaa kuyanyakua,

Deni hili walijua, utakuja kudaiwa ?

 

Makaa kuyanyakua, ya moto yaliyokuwa,

Ugumuwe wa mwamba, jabali lililokuwa,

Huko ukaungulia, kwa kushindwa itumia,

Deni hili walijua, utakuja kudaiwa ?

 

Mali yatahukumiwa, mwenzetu uliyopewa,

Vipi uliyatumia, sio tu kwa kujifaa,

Bali ni kwa manufaa, wengine waliokuwa,

Deni hili walijua, utakuja kudaiwa ?

 

Waliojilim bikia, ili yote kutumia,

Katikati kuishia, mzigo huuchukua,

Kweli wakaambiwa, imewakusanya dunia,

Deni hili walijua, utakuja kudaiwa ?

 

Utadaiwa na afya, wewe uliyoipewa,

Vipi ulititumia, binadamu kuwafaa,

Na wanyama nao pia, haki wataililia,

Deni hili walijua, utakuja kudaiwa ?

 

Cheo waliopatiwa,milki kutumikia,

Swali hawatakimbia, vipi walikitumia,

Nani kilichomfaa, pasina kupendelea,

Deni hili walijua, utakuja kudaiwa ?

 

Wakubwa waliokuwa, nguo watajazivua,

Dini walioikataa, userikali ukawa,

Nani walimtumikia, Mola wakamzulia,

Deni hili walijua, utakuja kudaiwa ?

 

Marais nao pia, wanafiki walokuwa,

Swali kuwashtakia, dhamana kuichezea,

Uongo wanapozua, watu wakasingizia,

Deni hili walijua, utakuja kudaiwa ?

 

Waliofata umbeya, haki wakapuuzia,

Yote kuzungumziwa, na mizani kupimia,

Kisha yakaamulia, kule kunakowafaa,

Deni hili walijua, utakuja kudaiwa ?

 

Michache imebakia, kutubu wanatakiwa,

Kaburi lajifungua, dhuluma kuziondoa,

Siku hiyo yaingia, wapaswa kuingojea,

Deni hili walijua, utakuja kudaiwa ?

 

Wabunge wa kutumia, fursa wataipewa,

Wao wakauliziwa, nani waliyemfaa,

Kama ndio wajilia, hukumu wajichongea,

Deni hili walijua, utakuja kudaiwa ?

 

Na walionunuliwa, bei watauliziwa,

Kiasi walopewa, watu wakajiuzia,

Na nchi kujinadia, fedha wakaichukua,

Deni hili walijua, utakuja kudaiwa ?

 

Viongozi watalia, dhuluma wakiijua,

Vipi watailipia, saa kuwageukia,

Na kilichowazuzua, muda hakikuchukua,

Deni hili walijua, utakuja kudaiwa ?

 

Maumbo waliyopewa, mazuri yaliyokuwa,

Nao watauliziwa, vipi waliyatumia,

Kama heri ilikuwa, faida kwao ikawa,

Deni hili walijua, utakuja kudaiwa ?

 

Uwezo waliopewa, la kwao litatakiwa,

Vipi waliutumia, katika hii dunia,

Kama waliuchezea, kilio wataangua,

Deni hili walijua, utakuja kudaiwa ?

 

Ujanja waliojaliwa, nao watauliziwa,

Kama watu ulifaa, au uliwaibia,

Kisha wakasiginiwa, motoni chini kukaa,

Deni hili walijua, utakuja kudaiwa ?

 

Akili waliopewa, nao watauliziwa,

Kwa mema walitumia, au ubaya kuzua,

Kisha wakahukumiwa, haki yao wakapewa,

Deni hili walijua, utakuja kudaiwa ?

No comments: