Tuesday, December 11, 2012

MSWAHILI


VIPI tutakuwa bora, watu tusipokosoa ?
Wakajifanya wakora, na ubabe kujitia,
Ninaona masihara, nchi tunaichezea,
Mswahili 'kimkosoa, hutaka kukumaliza:
Wala si kujiboresha !
Akajifanza ajua;
Na wewe kitu hujui!

Uganda iliborora, Amin kuipindua,
Mazuri akayagura, na kuulea ubaya,
Na kubwa kwao hasara, yeye kutomkosoa,
Mswahili 'kimkosoa, hutaka kukumaliza:
Wala si kujiboresha !
Akajifanza ajua;
Na wewe kitu hujui!

Amiri Mola hajawa, ni kiumbe hukosea,
Kwenye demokrasia, budi hili kumwambia,
Ila mkimuachia, udikteta mtalea,
Mswahili 'kimkosoa, hutaka kukumaliza:
Wala si kujiboresha !
Akajifanza ajua;
Na wewe kitu hujui!

Katiba husaidia, nyie mkijisaidia,
Hilo mkiliachia, anaweza ipindua,
Na yeye juu akawa, akaanza kufumua,
Mswahili 'kimkosoa, hutaka kukumaliza:
Wala si kujiboresha !
Akajifanza ajua;
Na wewe kitu hujui!

Wajanja humkalia, asiweze jiondoa,
Kisha wakamsukia, magumu kuyafumua,
Kila analoambiwa, yeye akaaminiwa,
Mswahili 'kimkosoa, hutaka kukumaliza:
Wala si kujiboresha !
Akajifanza ajua;
Na wewe kitu hujui!

Ulaya yalishatokea, leo China na Russia,
Na wenzake walokuwa, njia hii wapitia,
Ni uongo na hadaa, wengi wao wazaliwa,
Mswahili 'kimkosoa, hutaka kukumaliza:
Wala si kujiboresha !
Akajifanza ajua;
Na wewe kitu hujui!

Hutunga na kutungua, hakika yasiyokuwa,
Wakubwa wakiambiwa, kweli wakayadhania,
Kumbe kombamwiko wawa, siri chini wazitia,
Mswahili 'kimkosoa, hutaka kukumaliza:
Wala si kujiboresha !
Akajifanza ajua;
Na wewe kitu hujui!

Uongo nchi 'kilea, huwa mkubwa ukiwa,
Maamuzi huamua, uongo yalyojaa,
Kweli ikasanzuliwa, na uongo kuzagaa,
Mswahili 'kimkosoa, hutaka kukumaliza:
Wala si kujiboresha !
Akajifanza ajua;
Na wewe kitu hujui!

Unafiki utajaa, kila kona kuingia,
Hupika na kupakua, ya wengine kuzuia,
Hasidi mwana hadaa, fursa akachukua,
Mswahili 'kimkosoa, hutaka kukumaliza:
Wala si kujiboresha !
Akajifanza ajua;
Na wewe kitu hujui!

Uadui hukutia, mtu kwa kumkosoa,
Yako akayakataa, roho ngumu kujitia,
Hadi yakimuumbua, akabaini udhia,
Mswahili 'kimkosoa, hutaka kukumaliza:
Wala si kujiboresha !
Akajifanza ajua;
Na wewe kitu hujui!

Hapo nguvu huishia, kiburi kikabakia,
Akili zilivyofubaa, shindilia dona huwa,
Akawa akuzulia, sahihi lisilokuwa,
Mswahili 'kimkosoa, hutaka kukumaliza:
Wala si kujiboresha !
Akajifanza ajua;
Na wewe kitu hujui!

Hulilia kusifiwa, makosa kusahauliwa,
Mapambo akajitia, mzuri kufikiriwa,
Marashi ya Zanzibar, hadi nayo kuogea,
Mswahili 'kimkosoa, hutaka kukumaliza:
Wala si kujiboresha !
Akajifanza ajua;
Na wewe kitu hujui!

Harufu hatoitoa, mwilini hukomalia,
Jeraha likawa doa, milele kuendelea,
Na nchi ikaugua, kupona kazi ikawa;
Mswahili 'kimkosoa, hutaka kukumaliza:
Wala si kujiboresha !
Akajifanza ajua;
Na wewe kitu hujui!


No comments: