Saturday, December 29, 2012

Atakiwaye king'ora

Matumizi sijajua, king'ora kukitumia,
Laiti mkinambia, usahihi nitajua,
Wapi pa kukitumia, kugota nikaachia,
Atakiwaye king'ora, mgonjwa au mzima ?

Ni hoi aliyekuwa, kwa dhiki pia na njaa,
Au aliyejaliwa, tumbo limejifutua,
Shibe imemlevyea, hadi chakari akawa ?
Atakiwaye king'ora, hoi au alojaliwa

Kichanga aliyekuwa, njiani ameumia,
Au mkubwa kajaa, twatakiwa kumjua ?
Kwanza akajipitia, wengine tukafatia ?
Atakiwaye king'ora, mkubwa au mtogo ?

Nani wa mbele akawa, uchumi kuuinua,
Juu waliokalia, au chini walokuwa,
Wao wakinyanyuliwa, ngazi kwao kujakuwa ?
Atakiwaye king'ora, rais au raia?

Kibibi kashambuliwa, uchawi kutuhumiwa,
Au mzazi tarajiwa, zahanati kuwahia,
Aende kujifungua, kitumbe tusichojua?
Atakiwaye king'ora, mzazi au ajuza ?

Maiti zachukuliwa, mijifedha zashonewa,
Ipi tutakayojua, ni ujanja wa kuzuwa,
Njia tukawaachia, salama kujipitia ?
Atakiwaye king'ora, aliye hai au mfu ?

Akili zikizidia, hakika ujinga huwa,
Yapo ya kujirithia, twafaa kuyakataa,
Nendeni Scandinavia, haya mtajionea,
Atakiwaye king'ora, ni fedha au kiumbe ?

No comments: