Saturday, December 29, 2012

Mpe anayekunyima



Viumbe wana tabia, kufanyiana ubaya,
Ushauri nautoa, vitabu vyaniambia,
Wewe hivyo kutokuwa, lipa wema kwa ubaya,
Ushindi si kumnyima, mpe anayekunyima !

Shetani huwaingia, watu pasina kujua,
Roho kutojitambua, ubaya wakaulea,
Hata pasipowafaa, wajapo wakaumia,
Ushindi si kumnyima, mpe anayekunyima !

Roho tuliyoumbiwa, wema imetunukiwa,
Ubaya haikupewa, wala hautauzoea,
Bure mwaisingizia, nafsi inawahadaa,
Ushindi si kumnyima, mpe anayekunyima !

Mja ukishajijua, hili utalielewa,
Mbali ukalikimbia, mazuri kushikilia,
Na moja la kutmabua, lipa wema kwa ubaya,
Ushindi si kumnyima, mpe anayekunyima !

Ninakuhakikishia, wema ubaya waua,
Mtenda akaumia, hata machozi kutoa,
Kila akifikiria, dhuluma kakufanyia,
Ushindi si kumnyima, mpe anayekunyima !

Tenda paina ukiwa, moyo wako huru kuwa,
Deni ukatarajia, Allah unamwachia,
Kiumbe anaishiwa, sio yeye Adilia,
Ushindi si kumnyima, mpe anayekunyima !

Ukwasi amejaliwa, Swamadi mtunukiwa,
Mbingu na yote dunia, milki amechukua,
Hajui ya kuishiwa, wala  ya kupuhgukiwa,
Ushindi si kumnyima, mpe anayekunyima !

Viumbe wakulaaniwa, huwezi acha wajua,
Vidogo watagombea, na choyo kukufanyia,
Enenda wajichekea, hawajaijua dunia,
Ushindi si kumnyima, mpe anayekunyima !

Warithi kahadithia, nami nimekumbushia,
Sina nisichopekua, karibu na yeye nikawa,
Kwangu mimi ni ngekewa, nyingine nazikataa,
Ushindi si kumnyima, mpe anayekunyima !

No comments: