Monday, December 24, 2012

S I N E M A

Hakua kinachoanza, kikaacha kuishia,
Ndivyo ilivyo dunia, mwendo wake kwa hatua,
Awali kinachokua, akhiri humalizia,
Sinema zote huanza, na kisha zikaishia !

Nzuri inapokuwa, haraka huishilia,
Muda ukaudhania, unaifanya hadaa,
Pasina kujitambua, hatima ikafikiwa,
Sinema zote huanza, na kisha zikaishia !

Ukabaki washangaa, kama muda watimia,
watu ukashuhudia, wanaanza kujizoa,
Ndipo unapotambua, mwisho mmeshafikia,
Sinema zote huanza, na kisha zikaishia !

Ila mbaya 'kiingia, muda huwa watambaa,
Saa utaangalia, dakika haijaishia,
Kama unaye mbia, uwe kwake waugua,
Sinema zote huanza, na kisha zikaishia !

Muvii utaugulia, robo haijafikia,
Ukawa wajinyanyua, pengine kwenda ingia,
Kufanya usiojua, wala ya kujipangia,
Sinema zote huanza, na kisha zikaishia !

Kama uliitegemea, maliwazo kupatia,
Mja utatindikiwa, na hasira kuingia,
Kelele ukakataa, upwekeni kwenda kaa,
Sinema zote huanza, na kisha zikaishia !

Fikra zikakujia, lipi la kujifanzia,
Hakika lililokuwa, raha ukajipatia,
Mimi nimeligundua, nalo ninalitumia,
Sinema zote huanza, na kisha zikaishia !

Namtafuta Jalia, tena nikimlilia,
Maswali kumuingia, kila siku, kila saa,
Hakika nipate jua, jinsi anavyoamua,
Sinema zote huanza, na kisha zikaishia !

No comments: