Saturday, December 29, 2012

Huimbi lala mtoto



Mtoto sijasikia, lala mtoto kuimbiwa,
Hali sasa afungua, macho ili kuangalia,
Ataka changamkia, utoto kufurahia,
Huimbi lala mtoto, mwana akishaamka!

Kulala ukimwimbia, hilo haliwezi kuwa,
Lepe limemuishia, hawezi tena rudia,
Ila akijichokea, na njaa kutosikia,
Huimbi lala mtoto, mwana akishaamka!

Wakubwa mngelijua, wimbo huu udhia,
Mwana anapoimbiwa, aweza kukukwatua,
Au meno kukutia, pale usipotegemea,
Huimbi lala mtoto, mwana akishaamka!

Usingizi maridhia, kama alijipatia,
kwa miaka katulia, sasa ajiamkia,
Kukuru zake balaa, zaweza kuwaumbua,
Huimbi lala mtoto, mwana akishaamka!

Mkubwa akishakuwa, ni bora kumsikia,
Yake kuwaelezea, mkapata muelewa,
Elimu mngelitoa, hapa msingefikia,
Huimbi lala mtoto, mwana akishaamka!

Siasa kuzikimbia, kando mkajiwekea,
Kisha mkazungumzia, matumbo kujishibia,
Lugha hiyo waelewa, muafka hufikiwa,
Huimbi lala mtoto, mwana akishaamka!

Pamoja tungelikuwa, haya ningewaambia,
Mali yenu tunajua, kwa hapo ilipokaa,
Kwanza mnatakiwa, nyie mkajivunia,
Huimbi lala mtoto, mwana akishaamka!

Ila kwa wetu Utanzania,  sote budi kutufaa,
Mgao tutaangalia, mtakaokubalia,
Huo tutautumia, hadi neema kuenea,
Huimbi lala mtoto, mwana akishaamka!

Ujanja mkitumia, watu kuanza kugawa,
Mbali hamtafikia, kingoni mtatulia,
Mapya kuja zuliwa, hali mbaya kurejea,
Huimbi lala mtoto, mwana akishaamka!

No comments: