Monday, December 24, 2012

Mizizi nishaing'oa



YA UDIKTETA 'meng'oa, kidogo tu yabakia,
Shamba mikikazania, lote safi litakuwa,
Ila tu kama ikiwa, nanyi mtanunuliwa,
Mizizi nishaing'oa, uchafu kafagieni !

Kazi nilijitolea, mwenyewe kujifanyia,
Kizazi niweze faa, wasiukute udhia,
Magugu kushughulikia, taabu yatakayozua,
Mizizi nishaing'oa, uchafu kafagieni !

Enendeni mnajua, kupanda tu yabakia,
Mkiamua mvua, mnaweza kungojea,
Ila nimewachimbia, kisima cha kutumia,
Mizizi nishaing'oa, uchafu kafagieni !

Mwaweza kujilimia, pasina hiyo mvua,
Maji mkiyapakua, mnaweza kumwagiwa,
Kilimo kuendelea, bila ya kuachilia,
Mizizi nishaing'oa, uchafu kafagieni !

Haki mkiililia, uhuru sasa mkawa,
Ya uchumi kuamua, wenyewe kujifanyia,
Bila yakuwangojea, wajanja wa huko Daa,
Mizizi nishaing'oa, uchafu kafagieni !

Kuna nchi nawambia, ni ndogo kuliko mkoa,
Duniani zimejaa, uchumi wao wa paa,
Hil yetu ni dunia, kwa ukubwa yazidia,
Mizizi nishaing'oa, uchafu kafagieni !

Wamoja twaweza kuwa, ila  kwa kujitegemea,
Katikati tukakaa, ya pamoja kuyajua,
Ya uchumi si radhia, wasokwepo kuachiwa,
Mizizi nishaing'oa, uchafu kafagieni !

Haya yataka hatua, kila siku kuchukua,
Mashine tukatumia, ngamizi zilizokuwa,
Ikawa twafatilia, kwa usiku na mchana,
Mizizi nishaing'oa, uchafu kafagieni !

Haitulii dunia, na kulala ni balaa,
Sisi tukijilalia, tutakuja tawaliwa,
Miji inatakiwa, usingizi kukimbia,
Mizizi nishaing'oa, uchafu kafagieni !

Watu hujilalia, si kwa usiku kwingia,
Ila wakijichokea, nguvu zipate rejea,
Kisha wakendelea, mapinduzi kuyazua,
Mizizi nishaing'oa, uchafu kafagieni !

No comments: