Saturday, December 29, 2012

Kaolewe na benki



Naona yastahiki, benki wewe kukuoa,
Kwani wazidi hamaki, fedha kuipigania,
Kumbe wewe mamluki, na ndoana yako ndoa,
Kaolewe na benki, kiumbe usotosheka !

Senti waona ni haki,  sikuzote kupatiwa,
Hali hazitabiriki, siku katika dunia,
Yaliyokuwa afiki, nayo sasa yakataa,
Kaolewe na benki, kiumbe usotosheka !

Somo haufundishiki, wataka jana kwendelea,
Hilo haiyumkiniki, haliwezi kutokea,
Kama haubadiliki, kituo ninakijua,
Kaolewe na benki, kiumbe usotosheka !

Dunia ni ushiriki, kazi mkajipangia,
Na matumizi ya dhiki, wote mkayagundua,
Ili mjenge lukuki, njia zenye kuwafaa,
Kaolewe na benki, kiumbe usotosheka !

Tusiifanye hamaki, tukaja kujichongea,
Dunia haiaminiki, upendo wao wa riha,
Fakiri hathaminiki, wote watatukimbia,
Kaolewe na benki, kiumbe usotosheka !

Tunafaa kudiriki, tuanze kuzua mapya,
Tukimbie unafiki, kwa kesho kuangalia,
Nini lenye stahiki, linaweza kutufaa,
Kaolewe na benki, kiumbe usotosheka !

Nikiwa ni mabruki, haya  tutajivukia,
Mengi tukastahiki,  leo tusiyoyajua,
Ila huko hatufiki, kama leo twachezea,
Kaolewe na benki, kiumbe usotosheka !

No comments: