Monday, December 10, 2012

MANENO USHUZI MTUPU

Yachosha maneno tupu, sasa hatutasikiza,
Chukueni kwenye kapu, nyumbani kwenda kutunza,
Twataka marupurupu, kitaifa kujijaza,
Watu wataka vitendo, maneno yamewachosha!

Ndarahima hayajawa, maneno mengi udhia,
Vikombe vinapojaa, huja chini kuishia,
Mdomoni hutotia, sembuse kufurahia,
Watu wataka vitendo, maneno yamewachosha!

Nyuzi zitawaumbua, kwa habari kupotoa,
Uongo mkiulea, kaburi mwajichimbia,
Zama za kutokujua, sasa zimeishapotea,
Watu wataka vitendo, maneno yamewachosha!

Redio huwaumbua, vicheko wakaangua,
Tivii zikapwelea, ya kwenu kuyakogea,
Kisha wakawapakaa, uzushi mkiuzua,
Watu wataka vitendo, maneno yamewachosha!

Hotuba mkizitoa, viziwi kusikiliza,
Tena wanaosikia,  pamba wataziingiza,
Pasiwe la kuambua, ya kwenu wakayaiza,
Watu wataka vitendo, maneno yamewachosha!

Ya kwao mkiachia, yenu watayapoteza,
Taratibu huanzia, walii wakaeneza,
Hatua ikifikia, wenyewe mkajikwaza,
Watu wataka vitendo, maneno yamewachosha!

Watu watawakimbia, kama wakoma kufanzwa,
Mikono nyuma kutia, mbele kutotanguliza,
Mabega wakanyanyua, kama vile waapiza,
Watu wataka vitendo, maneno yamewachosha!

Nyuso watazichachua, kama limao wameza,
Pua wakazibetua, kama vile mmeoza,
Upange kuangalia, kama vile wawateza,
Watu wataka vitendo, maneno yamewachosha!

Kila mwenye kujijua, njia atajiuliza,
Safari iliyokuwa, ajapona kuteleza?
Ufupi uliokuwa, yepi atayamaliza?
Watu wataka vitendo, maneno .......yamewachosha!
BASI !!!!

No comments: