Saturday, December 29, 2012

Raia ni kama wana



ZAMA hizo tukijua, ungozi ni kulea;
Dhamana wakiitwaa; wao wazazi wakawa,
Leo tunawashangaa, wapitaji wamekuwa,
Raia ni kama wana, hivi ni mzazi gani:
Kizazi hukichukia:
Mwana humtakia mabaya;
Kisha akamsingizia;
Na kumtia  hatia ?

Wana wachanganyikiwa, njaa kuwashambulia,
Baba anakazania, shibe inawasumbua ?
Barazani amekaa, kiko anajivutia,
Raia ni kama wana, hivi ni mzazi gani:
Kizazi hukionea:
Akawalaza na njaa;
Na maji kuwamwagia;
Usiku wajilalia ?

Makombo awapatia, huko alikoyatoa,
Mashaka yanawatia, usalama kutokuwa,
Kuleni mkikataa, mtalala na njaa:
Raia ni kama wana, hivi ni mzazi gani:
Chakula huwaokotea,
Jalalani kwenye baa;
Sio kuwa kaishiwa;
Ila thamani kawatoa ?

Nje wakijitokea, ipate jua dunia,
Kuandamana balaa, mawe anawatupia,
Kisha kuwasingizia, ni wevi waliokuwa;
Raia ni kama wana, hivi ni mzazi gani:
Kizazi hukichukia:
Ulemavu kuwatia;
Kwa mabomu kurushia;
Na sumu kuwamwagia ?

Nje wakienda lia, ipate jua dunia,
Mkusanyiko huzua, maji moto kumwagiwa;
Kisha kuwasimbulia, sheria wanachezea;
Raia ni kama wana, hivi ni mzazi gani:
Kizazi hukichukia:
Ulemavu kuwatia;
Kwa mabomu kurushia;
Na sumu kuwamwagia ?

Mikataba aingia, urithi kujiuzia,
Wana wakiulizia, waambiwa kujijua;
Lao kujitafutia, malaika walokuwa ?
Raia ni kama wana, hivi ni mzazi gani:
Urithi ajinadia;
Bila wana kuwambia;
Mashimo yakabakia;
Kaburi kujichimbia!

Watu baki kaachia, mashamba wajivunia,
Senti anazoletewa, kila siku zinapwaya;
Mifuko imemjaa, hataki kujisumbua:
Raia ni kama wana, hivi ni mzazi gani:
Tathminiye hadaa;
Penye ukwasi pakiwa;
Mgeni hujichumia;
Wanawe  wakafulia ?

Akiambiwa hukataa, uongo akaridhia,
Hujifanzia sanaa, kwa akili kumjaa;
Kisha huwadithia, kile kisichowafaa,
Raia ni kama wana, hivi ni mzazi gani:
Kizazi hukichukia:
Ulezi akaondoa;
Hatari kuwatakia;
Wawapo katika njia  ?

Kwake kaifunga taa, gizani wana wakaa,
Vifaa ndani vyajaa, nishati ndio udhia,
Kila wakiililia, ni mchezo wachezewa,
Raia ni kama wana, hivi ni mzazi gani:
Gizani huwaachia:
Wakajihangaikia:
Yeye nuruni kakaa:
Vyake anavitumbua ?

Bomba kwake yaishia, maji kunywa ni ukiwa,
Wote wanahitajiwa, magoti kumpigia,
Jeuri ukijitia, kwa kiu utajifia;
Raia ni kama wana, hivi ni mzazi gani:
Maji kawadanganyia;
Na kiu kinawaua;
Wa nje awajazia;
Hadi wanayachezea ?

Asili yahukumiwa, sasa kusahauliwa,
Vijiji vinaumia, kwa kiu pia na njaa,
Nani wa kuangalia, wa mjini  wazidiwa ?
Raia ni kama wana, hivi ni mzazi gani:
Kijiji hukikimbia;
Mjini akaingia;
Kwake kupachukia;
Ustawi ukavia ?

No comments: