Monday, December 10, 2012

Heri ukawa mkosa


INGAWA waweza pewa, zote huwa zapotea,
Mikosi ikihamia, hapo kwako kuja kaa,
Au ukawa walewa, kwa mambo yake dunia,
Heri ukawa mkosa, lakini dhiki hauna!

Au ziwe zaingia, kisha ovyo zapotea,
Au wana wadokoa, wengine kuwagawia,
Pawe unachoopoa, ni mashaka kuingia,
Heri ukawa mkosa, lakini dhiki hauna!

Au mke kuwa mbaya, kwa fedha anapagawa,
Ndani akazichukua, nje kuwapelekea,
Pawe panachobakia, ni uchungu na kinaya,
Heri ukawa mkosa, lakini dhiki hauna!

Au wezi kuingia, shamba la bibi ukawa,
Kila ukijifungia, wajua pa kufungua,
Kitu kutokuachia, ila ni wako ukiwa,
Heri ukawa mkosa, lakini dhiki hauna!

Au kuzuka mabaa, na balaa kufatia,
Moto ukatokea, pasipo chanzo kujua,
Vingi kukuungulia, ukabaki umelewa,
Heri ukawa mkosa, lakini dhiki hauna!

Zikawaka motokaa, barazani zimekaa,
Kisa kutokitambua, na nani aliyezua,
Ukaichukia dunia, hadi ukachanganyikiwa,
Heri ukawa mkosa, lakini dhiki hauna!

Au zikenya mvua, hadi paa kuling'oa,
Jirani wakashangaa, mbona tu kwako yakawa,
Kinyamkera kikitua, chako kimeshachukua,
Heri ukawa mkosa, lakini dhiki hauna!

Maradhi ukaugua, waganga wasiojua,
Fedha ukazitumia,  Ulaya kwenda tibiwa,
Kila wakikuchungua, ugonjwa wawakimbia,
Heri ukawa mkosa, lakini dhiki hauna!

Darubini kufulia, viini vikapepea,
Sababu kutoijua, uchawi ukadhania,
Ramli ukiivaa, giza tupu latokea,
Heri ukawa mkosa, lakini dhiki hauna!

Mkosa akajaliwa,  apatacho kutumia,
Riziki ikamjia, bila ya  kujitambua,
Na afu akaridhia, neema iliyokuwa,
Heri ukawa mkosa, lakini dhiki hauna!

Mkosa akaridhia, kupata kuwa kinaya,
Moyo furaha kujaa, ukatoweka ukiwa,
Akazidisha na dua, kama maua kuchanua,
Heri ukawa mkosa, lakini dhiki hauna!

Yarabi muangalia, ya kwangu kuangalia,
Inanibeba dunia, yatosha ilivyokuwa,
Ziada nikiipewa, kwangu haijawa udhia,
Heri ukawa mkosa, lakini dhiki hauna!

No comments: