Monday, December 24, 2012

Imani ukichezea



Kuchezea endelea, nayo itakuchezea,
Wakati ukishawadia, hili utalitambua,
Subira imejaliwa, huvumilia dunia,
Imani ukichezea, nayo itakuchezea!

Utendi huwa hatua, na kauli ni hatia,
KIla ukishadidia, hesabu utaipewa,
Hatima ikiingia, katu haitopungua,
Imani ukichezea, nayo itakuchezea!

Haki ukiichezea, hubaki imetulia,
Yake kujikusanyia, siku ikaiongojea,
Ukijakushtukia, milima imeshakuwa,
Imani ukichezea, nayo itakuchezea!

Usawa pasipokuwa, uwizi hupaliliwa,
Ya wengi kutwaliwa, wachche wakachukua,
Kisha wakajifungia, vya wizi kwangalia,
Imani ukichezea, nayo itakuchezea!

Imani yavumilia,  kiu hata pia njaa,
Polepole hujongea, haraka haitakimbia,
Ila yake inajua,  wala haitayaachia,
Imani ukichezea, nayo itakuchezea!

Ujinga ukijitia, mwenyewe utajikwaa,
Siku wakijaamua, maiti kuikataa,
Na wako wakaambiwa, waende kujizikia,
Imani ukichezea, nayo itakuchezea!

Au mamluki wakawa, ndio uloandikiwa,
Dini wasiojua, kama mfu kufukiwa,
Hesabu ikaishia, pale ulipoanzia,
Imani ukichezea, nayo itakuchezea!

No comments: