Saturday, December 29, 2012

Imani sio kelele

 
Imani wasiokuwa, kwa kelele huwajua,
Itarindima  mitaa, eti wanafurahia,
Na kundini kujitia, Mola wanamhofia,
Imani sio kelele, wengine kuwapigia !
 
Kumbe kwao ni mzaha, usanii wajitia,
Yao wamejilengea, kutimu wakusudia,
Nao wasiotambua, mkengeni huingia,
Imani sio kelele, wengine kuwapigia !
 
Miziki huifungua, masikio kuvamiwa,
Ugaidi kufanyia, ushindwe jipumzikia,
Ni furaha ya hadaa, masaa haitachukua,
Imani sio kelele, wengine kuwapigia !
 
Udamisi hujitia, marafiki  kununua,
Pilau kuwapikia, kula pamoja kwa furaha,
Nje wakichekelea, ndani uovu wajaa,
Imani sio kelele, wengine kuwapigia !
 
Si heri hapo hutua, ila bad na majaa,
Watu wakijiondoa, wengine wakaugua,
Na mikosi kufatia, kila wanakopitia,
Imani sio kelele, wengine kuwapigia !
 
Mwaka hawataujua, ndondocha  watazaliwa,
Yao hapo kuishia, wao wakaendelea,
Nyumba usiyoijua, ogopa kwenda kukaa,
Imani sio kelele, wengine kuwapigia !
 
Kuna nyumba za nazaa, uovu zinazolea,
Mchana utadhania, walokole wamekua,
Usiku ukiingia, mashetani wanakuwa,
Imani sio kelele, wengine kuwapigia !
 
Roho wanazojaliwa, nyeusi zanyaukia,
Hata weupe wakiwa, dalili huzihofia,
Wewe hawatakwambia, kwingine huzungukia,
Imani sio kelele, wengine kuwapigia !
 
Furqani maridhia, kinga ninakutumia,
Enenda kuwaumbua, popote wanapokaa,
Na usiku wakitua, kaziyo kuwanyanyua,
Imani sio kelele, wengine kuwapigia !
 

No comments: