Monday, December 24, 2012

Uhuru wa kiuchumi



Katika hii dunia, kuna nchi nawambia
Ndogo kuliko mikoa, zinazidi kupasua,
Kweli wao wakimbia, hali sisi twatembea,
Uhuru wa kiuchumi, mikoani lilieni!

Milioni kutimia, wengi hawajafikia,
Ila wanayojifanyia, utadhania dunia,
Dhiki wamezikimbia, hadithi husimuliwa,
Uhuru wa kiuchumi, mikoani lilieni!

Ukubwa waliozoea, ni wagumu kuachia,
Uzito wanadhania, na ukubwa wazaliwa,
KIsha yanayotokea, kila kona kufulia,
Uhuru wa kiuchumi, mikoani lilieni!

Ushindani wavia, hakuna kwenye mikoa,
Juu waliokuwa, yao wanajifanyia,
Si wa kuchaguliwa, nani atawaondoa?
Uhuru wa kiuchumi, mikoani lilieni!

Mitaji wameamua, kuigeuza mikoa,
Kwanza wao waanzia, ndugu zao hufatia,
Na rafiki na jamaa, mwaliko wakaupewa,
Uhuru wa kiuchumi, mikoani lilieni!

Haina jipya mikoa, yale yale yanakuwa,
Miongo inaishia, hali ile ile yawa,
Mingine inasinyaa, upya inapozaliwa,
Uhuru wa kiuchumi, mikoani lilieni!

Mipango inatakiwa, kompyuta kuwekewa,
Hapo hapo kufatiwa, kwa dakika na masaa,
Yale ya kuyangojea, Daa imeshachelewa,
Uhuru wa kiuchumi, mikoani lilieni!

Harakati zatakiwa, jikoni kushughulikiwa,
Vipi kwenda kupikiwa, sebuleni pa kukaa,
Hili tukilitambua, ustawi watujia,
Uhuru wa kiuchumi, mikoani lilieni!

No comments: