Tuesday, December 11, 2012

Chini kunaterereka

Juu wameshikilia, meli bado yatembea,
Ni nzima  watwambia, hakuna la kuhofia,
Ila chini tunajua, maji yaanza ingia,
Chini kunaterereka, huko juu ni salama ?

Mitambo inafulia, na nguvuze kupungua,
Kasi yazidi pungua, na uzito kuzidiwa,
Kioja kinatokea, mamluki kuingia,
Chini kunaterereka, huko juu ni salama ?

Rushwa inajiotea, majabalini kukua.,
Kwa ukame kuzidia, na njaa kuota jua,
Uchama sasa sanaa, wajinga kununuliwa,
Chini kunaterereka, huko juu ni salama ?

Nyufa saruji zatiwa, mirija inakataa,
Haiwezi kuingia, nje wakajinyonyea,
Na wanaoandaliwa, ktu hawajasomea,
Chini kunaterereka, huko juu ni salama ?

Hayati wafufuliwa, uhai kuja kutia,
Akili zilishapoa, hii si yao dunia,
Yacheza teknolojia, wajanja kuya nyolewa,
Chini kunaterereka, huko juu ni salama ?

Harabu yaendelea, hujuma kwao ridhaa,
Mbio wanazitumua, filimbi hawajasikia,
Bastola ikilia, wao wameishasanzua,
Chini kunaterereka, huko juu ni salama ?

Athari inaenea, pasi mtu kukemea,
Hali waikubalia, inabidi kuilea,
Mwana mwizi mwamjua, aletavyo mwapokea ?
Chini kunaterereka, huko juu ni salama ?

Gari wameshaondoa, sio wa kwasikia,
Huko walikofikia, upepo wameshalewa,
Chini wakijatulia, hakuna pakukanyagia,
Chini kunaterereka, huko juu ni salama ?

Mizizi ikisambaa, vijijini kuingia,
Hofu wataiondoa, mbadala kuridhia,
Ila kinachotakiwa, matatizo kutatua,
Chini kunaterereka, huko juu ni salama ?

Ila kinachotakiwa, matatizo kutatua,
Kama maji kufumbua, jinsi ya kuwapatia,
Neema ikishaingia, watu huru watakuwa,
Chini kunaterereka, huko juu ni salama ?

No comments: