Monday, December 24, 2012

Ujinga

Ushauri ukipewa, kachukue mizania,
Upime na kupumua, na tafakuri kutia,
Sio ukajizolea, kisha kujiropokea,
Akikushauri mjinga, ujinga, na wewe mjinga!

Katika hii dunia, kuna wapishi wa midia,
Kazi wanayoipewa, uoza kuufukia,
Hela marashi hutia, uzuri ukanukia,
Akikushauri mjinga, ujinga, na wewe mjinga!

Wajinga wamezaliwa, ushauri kuutoa,
Na wanaowasikia, ujinga huuchukua,
Kwayo yao kuamua, ujingani huingia,
Akikushauri mjinga, ujinga, na wewe mjinga!

Kasma ukishapewa, mtu ni kukadiriya,
Jambo kutoliogea, hadi umelichungua,
Ukweli ukaujua, na kiini kuagua,
Akikushauri mjinga, ujinga, na wewe mjinga!

Mambo ukiyasikia, kweli ukahesabia,
Kitanzi unajitia, na heshima kuivua,
Waweza kuadhiriwa, mitihani ukipewa,
Akikushauri mjinga, ujinga, na wewe mjinga!

Inatakiwa tabia, kiasi kujijengea,
Ikawa ni mazoea, haki kuipalilia,
Daima hii dunia, hulemea wenye njaa,
Akikushauri mjinga, ujinga, na wewe mjinga!

Akili kutoachia, nyumayo zikabakia,
Mbele zikisogea, zaweza kusaidia,
Kauli ukiitoa, upate kuheshimiwa,
Akikushauri mjinga, ujinga, na wewe mjinga!

Vinginevyo hulaniwa, ushenzini ukatiwa,
Pasiwe kuaminiwa, bali ni mbovu bidhaa,
Pembeni ukafagiwa, uonekane kinyaa,
Akikushauri mjinga, ujinga, na wewe mjinga!

No comments: