Tuesday, December 11, 2012

Asiyevaa vazi hili



HILO ni vazi la takwaa, latakiwa kuvaliwa,
Ukuu wanaopewa, huruma wakaipewa,
Wezi wakikimbilia, ni hasara kubwa huwa,
Asovaa vazi hili, daima uchi hubaki !

Walaji wakiingia, vya watu watajilia,
Dhuluma wakaizaa, na kisha wakailea,
Kizima kitaugua, au ulemavu kutiwa,
Asovaa vazi hili, daima uchi hubaki !

Hawajengi hubomoa, hadi paa kuezua,
Msiba mkubwa ukawa, wafuasi kuuawa,
Moyoni wakauawa, na imani kupotea,
Asovaa vazi hili, daima uchi hubaki !

Fasidi wakijitia, mali zitawaumbua,
Kisicho chao kutwaa, vingine wakatumia,
Na ya wengi manufa, ya mmoja tu yakawa,
Asovaa vazi hili, daima uchi hubaki !

Wakijaa changudoa, ombaomba wote huwa,
Kisha mapambo wakawa, ya ukubwa kupambiwa,
Taadhima hujifia, ugoni ukakohoa,
Asovaa vazi hili, daima uchi hubaki !

Ombaomba wakijaa, rushwa wataipokea,
Huwa ni yao fidia, pasina kufikiria,
Yao wakajiuzia, almasi vilokuwa,
Asovaa vazi hili, daima uchi hubaki !

Yao wakajiuzia, almasi vilokua,
Na ksiha wakalilia, shanga kwenda gaiwa,
Inacheka Tanzania, Afrika inalia,
Asovaa vazi hili, daima uchi hubaki !

Yasikitika dunia, uongozi kufulia,
Zama zilizokuwa, nchi  ikiheshimiwa,
Mwalimu alililiwa, leo twajishobodoa,
Asovaa vazi hili, daima uchi hubaki !

Sasa twajifaragua, hata tusipokusudiwa,
Mwaliko kujigawia, na wala si kuletewa,
Pumzi zimetuishia, tumebakia gunia,
Asovaa vazi hili, daima uchi hubaki !

Mbadala wakataa,  vichuguu vyaeneea,
Mola tumemtezea, na yeye atuwatia,
Kwa kujitia twajua, aone tunachoambua,
Asovaa vazi hili, daima uchi hubaki !

Wachache wakitokea, hali wakamlilia,
Mwepesi wa kusikia, ya watani kuyajua,
Hawezi kutukimbia, pasi ngao kubakia,
Asovaa vazi hili, daima uchi hubaki !

Usafi tukijitia, tena atatuangalia,
Wajihi kutwangalia, na moyowe kufungua,
Aipenda Tanzania, uongo isiyokuwa,
Asovaa vazi hili, daima uchi hubaki !

No comments: