Saturday, December 29, 2012

Uziwi wanajitia



ZAMA zimetufikia, ngoma zetu kutoboa,
Ukadhani wajijua, na kuwakoga jamaa,
Anga ukazipasua, riha ipate enea,
Uziwi wanajitia, kwa wengine kusumbua!

Kumbe unajishaua, ubaya kukurudia,
Masikio kutoboa, uziwi ukaingia,
Siku inapofikia, muziki hutoujua,
Uziwi wanajitia, kwa wengine kusumbua!

Kelele lhutoijua, tofauti ilokuwa,
Muziki kilingania, sawa ukajionea,
Midadi uloringia, ikawa yakuumbua,
Uziwi wanajitia, kwa wengine kusumbua!

Hali sawa kujitia, njiani ukitembea,
Ila kwa wanaokujua, vidole kukunyoshea,
Watu wakahadithia, kisa kilichotokea,
Uziwi wanajitia, kwa wengine kusumbua!

Ulikuwa wa kujua, ngoma unajijazia,
Za uzito kadiria, disco unaoingia,
Ndani ukajichimbia, ili watu kustua,
Uziwi wanajitia, kwa wengine kusumbua!

Lakini haukujua, mzizi unachimbua,
Vifaa kuvipasua, visije kesho kufaa,
Wakati ukafikia, si tena wa kusikia,
Uziwi wanajitia, kwa wengine kusumbua!

Dhihaka uliyogawa, iwe inakurudia,
Furaha uliyojua, ikaja kuwa ni ukiwa,
Dhiki kutojitambua, ukiishi na jamaa,
Uziwi wanajitia, kwa wengine kusumbua!

Wakwasi waliopewa, wazazi wajivunia,
Wana wakawaachia, wakaitesa jamaa,
Nayo kama hayo pia, ndiyo yanayowafikia,
Uziwi wanajitia, kwa wengine kusumbua!

No comments: