Saturday, December 29, 2012

Kila kitu kina hadhi



Hakuna asiyejua, thamani kapungukiwa,
Mzawa adharauliwa, hadhi amefilisiwa,
Wakuu washindania, tena chini kumtia,
Kila kitu kina hadhi, ila mzawa nchini!

Uwizi anahofia, vya watu kuvikwapua,
Na wanaosingizia, ushahidi waishiwa,
Maneno yanabakia, huku wana waugua,
Kila kitu kina hadhi, ila mzawa nchini!

Uvivu asingiziwa, na ruksa kulilia,
Wakubwa wayasikia, wawekezaji kwmbia,
Yao wakayaridhia, la mzawa kukataa,
Kila kitu kina hadhi, ila mzawa nchini!

Elimu wanfulia, na ujuzi una njaa,
Hivyo wanatenguliwa, uboi ndio wafaa,
Na usafi kuutia, vyumba vikapendezea,
Kila kitu kina hadhi, ila mzawa nchini!

Umeneja wachagua, nje wanaotokea,
Haramu wakaingia, na bado waajiriwa,
Udhibiti wafulia, nini wanalolijua ?
Kila kitu kina hadhi, ila mzawa nchini!

Au wameshachukua, mapema walichong'oa,
Macho wakajifumbia, ujingani kujitia,
Mchezo kwako wachezewa, wachezaji kutojua?
Kila kitu kina hadhi, ila mzawa nchini!

Mwka huu natulia, yangu nimeelezea,
Kazi hayajafanyiwa, majibu nayangojea,
Kitu sikuambulia, bali macho kufungua,
Kila kitu kina hadhi, 'sipokuwa Mtanzania!

No comments: