Saturday, December 29, 2012

Siasa kwenye ulaji


 

Thamaniye huwa chini, miguu ikafutiwa,

Na popote duniani, nafasi haitapewa,

Mengine huwa utani, tumbo likichaguliwa,

Siasa kwenye ulaji, miguu itafutiwa!

 

Hata wenye kampuni, hili wanaliewa,

Fayageti huwa duni, watu wakajipitia,

Kwani upo ushindani,  njia wajitafutia,

Siasa kwenye ulaji, miguu itafutiwa!

 

Huondoka mashakani, mageti wakiyatia,

Ninajua yumkini, wapo rushwa wapokea,

Wataniachia ndani, kazi nikajifanzia,

Siasa kwenye ulaji, miguu itafutiwa!

 

Mla kala leo kwani, hili hawajalijua,

Na msomi wa mizani, huwa ametangulia,

Anayetamba nyikani, na mjini akujua,

Siasa kwenye ulaji, miguu itafutiwa!

 

Hutamba kwayo hisani, walaji wanayotoa,

Hali zetu bado guni, daawa haijatua,

Na ndarahima sineni, wingiwe sijaujua,

Siasa kwenye ulaji, miguu itafutiwa!

 

Ila sio yumkini, wote watazimwagiwa,

Hizo zina matawini, pamo namo mwa mitaa,

Kiasi chake mizani, imeishakutulia,

Siasa kwenye ulaji, miguu itafutiwa!

 

Hapa nilikuwa ndani, yangu nishajifanyia,

Ninawaaga watani, mwakani nitarejea,

Kwa leo pumzikeni, inshallah tukirejea,

Siasa kwenye ulaji, miguu itafutiwa!

 

Nilitoka bustani, maua kujipandia,

Kuingia kilingeni, mikwara nikaivaa,

Karibu sikubaini,  nje ninazuiliwa,

Siasa kwenye ulaji, miguu itafutiwa!

 

Nikakusanya watani, kazi wakaigombea,

Muda sikuubaini, saa gani ilikuwa,

Sikuona ubishani, dau nikajipangia,

Siasa kwenye ulaji, miguu itafutiwa!

 

Nikafungua vipini, na funguo kuzitoa,

Kisha nikawa makini, njia yangu kuchagua,

Pale kwenye upinzani, kupita nikakataa,

Siasa kwenye ulaji, miguu itafutiwa!

 

Pasipo na upinzani, nikazishusha silaha,

Sikupanda ukutani, mlangoni mepitia,

Nilipojitoma ndani, sera nikazipangua,

Siasa kwenye ulaji, miguu itafutiwa!

 

Kumbe hivi umaskini, kwa wngine ni silaha,

Hili wanalithamini, wataka kuendelea,

Ukifikia mwishoni, wapo wengi kufulia,

Siasa kwenye ulaji, miguu itafutiwa!

 

Na kisha abauitani, utajiri ndiyo njia,

Huna watalokuhini, fukara walia njaa,

Yako watayaamini, na njia kukuachia,

Siasa kwenye ulaji, miguu itafutiwa!

 

Yaoneni ya kusini, nako mashariki pia,

Uongozi wa imani, wafa kama ujamaa,

Sasa twabaki manyani, kuiga waliokuwa,

Siasa kwenye ulaji, miguu itafutiwa!

 

Watu hawana thamani, kitu wasipojaliw,a

Daima wakawa chini, watu wa kuitikia,

Ukubwa ni wa mizani, uzito ukachukua,

Siasa kwenye ulaji, miguu itafutiwa!

 

Vyama viko mashakani, yaoza demokrasia,

Imetiwa mitihani, migumu kujivukia,

Pasina ya mabilioni, ona vinavyougua,

Siasa kwenye ulaji, miguu itafutiwa!

 

Wafuasi wa imani, wote wameshazolewa,

Wanabaki mumiani, senti kuzifuatilia,

Walojaa mfukoni, miungu wameshakuwa,

Siasa kwenye ulaji, miguu itafutiwa!

 

Chama chao maskini, matajiri wachukua,

Wabakie mitaani, hadithi kusimulia,

Hawanao ushindani, wenye fedha watambia,

Siasa kwenye ulaji, miguu itafutiwa!

 

Nazo hizi kampuni, za simu zilizokuwa,

Se zetu tulio duni, wenye nacho wametwaa,

Yao kama ni shakani, rahisi kukuzuia,

Siasa kwenye ulaji, miguu itafutiwa!

 

Wafanza kama hisani, huku wanakupakua,

Wakakukata mapeni, muda wakakukatia,

Mnyonge ufanye nini, kwa waua demokrasia?

Siasa kwenye ulaji, miguu itafutiwa!

No comments: