Saturday, December 29, 2012

Uchochezi ndio nini

Uhaini ndio nini, pakiwepo ushindani,
Wanasheria watani, naomba lizungumzeni,
Latutia matatani, sisi tusiobaini,
Uchochezi ndio nini, dunia ya ushindani?

Niandike kitu gani,  uchochezi kutoghani,
Kama maji siyaoni, niseme yako njiani,
kama twaishi gizani, niige niko nuruni ?
Uchochezi ndio nini, dunia ya ushindani?

Kama shibe siioni, niseme niko makini,
Njaa iko hatarini, kuilaza kaburini,
Nitamdanganya mtu gani, kati ya walioko ndani ?
Uchochezi ndio nini, dunia ya ushindani?

Hata kichanga sidhani, baba kitaniamini,
Kitaniona ni mhuni, kama sio mamluni,
Akishanitathmini, akanitoa hisabuni,
Uchochezi ndio nini, dunia ya ushindani?

Nitakuwa hayawani, wengi wasiniamini,
Au kuwa utumwani, shaka watia moyoni,
Jamani niambieni, uchochezi kitu gani ?
Uchochezi ndio nini, dunia ya ushindani?

Haki zetu kubaini, nisiseme hadharani,
Katiba nisiamini, uhuru kunipa thani ?
Nizungumze kwa yakini, haki hata kwa maskini,
Uchochezi ndio nini, dunia ya ushindani?

Zama zenye ushindani, yote naona ilani,
Yategemea maoni, we, uko upande gani,
Hili ukitathmini, uhaini, uzaini,
Uchochezi ndio nini, dunia ya ushindani?

Mawakili elezeni, mna msimamo gani,
Na sisi tujiamini, pasina kuwa haini,
Itengezeni mizani, pande zote kuauni,
Uchochezi ndio nini, dunia ya ushindani?

No comments: