Monday, December 24, 2012

F U R A H A

Hili nimeligundua, na wala sikushangaa,
Zama nikiulizia, nini wanachekelea,
Nikaja kulitambua, la kuiga limekuwa,
Kuna furaha nyingine, kumbe huwa ni bandia?

Kicheko hukiangua, mtaa ukasikia,
Kitu ukiangalia, wala hutajionea,
Furaha ukadhania, wenzako wamejaliwa,
Kuna furaha nyingine, kumbe huwa ni bandia?

Hucheka hadi kulia, na miguu kusugua,
Nguzo zikakumbatiwa, na pombe kujimwagia,
Pepo ukatabiria, tayari wameingia,
Kuna furaha nyingine, kumbe huwa ni bandia?

Hao hao hutokea, siku wakakushtua,
Kibao wamenyanyua, wenzi kuwageuzia,
Matusi wanayotoa, choo marashi hutoa,
Kuna furaha nyingine, kumbe huwa ni bandia?

Husimangwa wa kupewa, na visa kusimbuliwa,
Wazi akaadhiriwa, kama nguo avuliwa,
Rafiki aliyekuwa, mara adui akawa,
Kuna furaha nyingine, kumbe huwa ni bandia?

No comments: