Monday, December 10, 2012

K A B U R I



WAKUBWA twawaombeni,  hadithi zisikizeni,
Vyanzo viangalieni, yao msikubalini,
Watuweka hatarini, tena hatuna imani,
TANESCO ni kaburi, la mizimu ya fisadi:
Litaonoka na wengi!

Salamu za nuksani, mwaka mpya waghani,
Wasivyokuwa makini, kutuchafua moyoni,
Uungwana siuoni, ila uroho azani,
TANESCO ni kaburi, la mizimu ya fisadi:
Litaonoka na wengi!

Kaburi hili oneni, lingali wzi jamani,
Laita usingizini, hili mngelibaini,
Wataondoka wandani, hima sasa fukieni,
TANESCO ni kaburi, la mizimu ya fisadi:
Litaonoka na wengi!

Aushi yao si auni, ladidimia thamani,
Wamekua mumiani, damu kunyonya nchini,
Kisha kuwapa wageni, sisi twakosa thamani,
TANESCO ni kaburi, la mizimu ya fisadi:
Litaonoka na wengi!

Na sasa waambieni, gharama kapunguzeni,
Na ya uwizi madeni, nyie kayaondoeni,
Mwaichezaa amani, hivi hili hamuoni?
TANESCO ni kaburi, la mizimu ya fisadi:
Litaonoka na wengi!

Hasira zetu angani, nje sasa zioneni,
Mnatufanzia utani, nafuu hatuioni,
Mwapitia chuo gani, bei kutorudi chini ?
TANESCO ni kaburi, la mizimu ya fisadi:
Litaonoka na wengi!

Wachache ng'ombe mjini, hamuendi vijijini,
Asilimia ishirini, zaidi msitukamueni,
Huduma zenu ongezeni, na wigo upanueni,
TANESCO ni kaburi, la mizimu ya fisadi:
Litaonoka na wengi!

Ovataimu punguzeni, mmezidisha uhuni,
Dakika mnasaini, siku nzima kazini,
Unyafuzi mtihani,  mwataka tuwashukieni ?
TANESCO ni kaburi, la mizimu ya fisadi:
Litaonoka na wengi!

Teknolojia yakini, itumike shirikani,
Mikwara ipunguzeni, gharama ziondoeni,
Na magari naamini, mzigo kwa kampuni,
TANESCO ni kaburi, la mizimu ya fisadi:
Litaonoka na wengi!

Uingereza enendeni,habari mkapateni,
Gavana wao benkini, kuwa Mark Carney,
Si Mwingereza jamani, Canada kwao

nyumbani,
TANESCO ni kaburi, la mizimu ya fisadi:
Litaonoka na wengi!

Wazawa naona duni, kuongoza shiriikani,
Sera kaitungeni, ya kumpata mgeni,
Sio kwa janja na uhuni, wakaguzi tumieni,
TANESCO ni kaburi, la mizimu ya fisadi:
Litaonoka na wengi!

Kuna mashirika nchini, mzawa huywa shakani,
Kuongoza mtihani, upesi watamzaini,
Siasa ikawa ndani, hata mbele hakuoni,
TANESCO ni kaburi, la mizimu ya fisadi:
Litaonoka na wengi!


Waachieni wageni, mapya watufundisheni,
Aliyezaliwa gizani, ataipa nuru kampuni ?
Na mtoto wa kijijini, TANESCO itamthamini?
TANESCO ni kaburi, la mizimu ya fisadi:
Litaonoka na wengi!

Viongozi wahisani, mikakati mbaini,
Wakuu wa mikoani, dhima hii kawapeni,
Njia zao wabaini, umeme afu kondeni,
TANESCO ni kaburi, la mizimu ya fisadi:
Litaonoka na wengi!

TPC kayaoneni, aidha Njombe miwatini,
Njia wameshazibuni, wazalisha vijijini,
Mimi hili naamini, lisingojee karni,
TANESCO ni kaburi, la mizimu ya fisadi:
Litaonoka na wengi!

Mbadala mbaini, kwa mjini na vijijini,
Umeme kitu makini, kuondoa umaskini,
Na hatari za nyumbani, daima huenda chini,
TANESCO ni kaburi, la mizimu ya fisadi:
Litaonoka na wengi!

Wataraji wahisani, leo tungekuwa mwangani,
Watushangaa amini, kuona tuko gizani,
Hili hawaliamini, mchawi wetu ni nani?
TANESCO ni kaburi, la mizimu ya fisadi:
Litaonoka na wengi!

Tuonoze Maanani, kawi isiwe shakani,
Utujenge akilini, na kutuponya moyoni,
Uoza ukibaini, uutupe vichakani,
TANESCO ni kaburi, la mizimu ya fisadi:
Litaonoka na wengi!

No comments: