Monday, December 24, 2012

Hujui pa kumuweka ?

Mnaloliazimia, katu haliwezi kuwa,

Nyie mkajipandia, chini mola kumwachia,

Dunia atapindua, juu chini kwenda kuwa,

Mungu hatokuwa chini, tamaa zitawaponza !

Mcheza mwamchezea, asije kuwabetua,

Kitu hamtabakia, ila kulizwa  ukiwa,

Walikuwa walokuwa, hivi nyie mtakuwa?

Mungu hatokuwa chini, tamaa zitawaponza !

Ndiye mwenye kuenea, kote anayetembea,

Katikati anakaa, kushoto pia kulia,

Saa zote katulia, dunia aiangalia,

Mungu hatokuwa chini, tamaa zitawaponza !

Sio wa kujisumbua, huisumbua dunia,

Upweke sio tabia, watumishi wamejaa,

Wazunguka na kupaa, waendako akujua,

Mungu hatokuwa chini, tamaa zitawaponza !

Saa akadiria,  umri waliojaliwa,

Muda haitochukua, wengine wakaingia,

Walio kwenye dunia, miaka wakadhania,

Mungu hatokuwa chini, tamaa zitawaponza !

Hao huwaangalia, kitu wasiotambua,

Wao wakajipangia, kuikusanya dunia,

Yeye akayapangua, wote akajikusanyia,

Mungu hatokuwa chini, tamaa zitawaponza !

Firauni kawania, uungu kuuchukua,

Muda mwingi akapewa, toba apate kutoa,

Ujibari kajitia, hata watu kuwaua,

Mungu hatokuwa chini, tamaa zitawaponza !

Siku ilipowadia, bahari ikajinywea,

Matapishi kuyatoa, pembeni akatupiwa,

Na leo amebakia, ushahidi kwa dunia,

Mungu hatokuwa chini, tamaa zitawaponza !'

Wengi wametangulia, na wengi wamefatia,

Hatima yao ikawa, hiyo hiyo ilokuwa,

Wingi wanaomtia, hukumu moja ikawa,

Mungu hatokuwa chini, tamaa zitawaponza !

Haachi kutuambia, astahili abudiwa,

Mmoja aliyekuwa, pasina kusingiziwa,

Laana keshaitoa, wote wataangamia,

Mungu hatokuwa chini, tamaa zitawaponza !

No comments: