Friday, November 2, 2012
Chanzo usipokijua
MARADHI ukiugua, vyema kiini kujua,
kama usipokijua, bure unajisumba,
Weza ukasingizia, ugonjwa usiougua,
Chanzo usipokijua, mtabaki hangaika !
Weza ukasingizia, ugonjwa usiougua,
Dawa ukazitumia, sahihi zisizokuwa,
Rangi kuwa kahawia, au zambarau ukawa,
Chanzo usipokijua, mtabaki hangaika !
Mambo ya kuyasikia, bila ya kujionea,
Ni umbeya kuulea, Daudi aliambiwa,
Lawama zikiingia, ushahidi watakiwa,
Chanzo usipokijua, mtabaki hangaika !
Ushahidi watakiwa. upande mshtakiwa,
Na yeye kuelezea, jinsi ilivyotokea,
Mmoja ukiiusikia, haki inahujumiwa,
Chanzo usipokijua, mtabaki hangaika !
Mashahidi watakiwa, huru wanaotambuliwa,
Pande wasiolalia, na cha mbele kuchukua,
Adili waliojaliwa, na utu wanaojua,
Chanzo usipokijua, mtabaki hangaika !
Sio wa kuwanunua, mfukoni walotiwa,
Imani mfu ikawa, na haya inshapotea,
Wasafi wanatakiwa, kote wakaaminiwa,
Chanzo usipokijua, mtabaki hangaika !
Chanzo watu wanazua, kingine kikaja kuwa,
Uongo wenye hadaa, ya matumbo yenye njaa,
Wapikwa na kutumiwa, waso aibu wapewa,
Chanzo usipokijua, mtabaki hangaika !
Chanzo ukweli chajua, halali kinapokuwa,
Si dalili kudhania, ndio kiini kimekua,
Kosa utaliingia, uwe wa kulaumiwa,
Chanzo usipokijua, mtabaki hangaika !
Chanzo kama mshumaa, au hata bora taa,
Nuru huwa kinatoa, palepale ukajua,
Vinginevyo ikiwa, unaicheza nazaa,
Chanzo usipokijua, mtabaki hangaika !
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment