Sunday, November 18, 2012
KIONGOZI WA UKWELI
ZAMA za kujilimbia, zafaa wasiojijua,
Karibu wa kuangalia, wasiojua dunia,
Kitu wasiosikia, ila kujaliwa raha,
Kiongozi wa ukweli, hatojishibisha kwanza:
Huwashibisha raia.
Wa kweli anayekua, kula atajachelewa,
Mbele hatakimbilia, na sinia kachukua,
Ila nyuma atakaa, kikombe kakumbatia,
Kiongozi wa ukweli, hatojishibisha kwanza:
Huwashibisha raia.
Hatopenda kutumia, kwa kuwa nchi yatoa,
Mbali hatakimbilia, karibu kuangalia,
Watu hatosaidia, ila uwezo kuvua,
Kiongozi wa ukweli, hatojishibisha kwanza:
Huwashibisha raia.
Si wa kusimulia, ya watu kuyasikia,
Huchuja kwa hilo kawa, na vichujio kadhaa,
Yote akaangalia, kwa pembe zenye kuzua,
Kiongozi wa ukweli, hatojishibisha kwanza:
Huwashibisha raia.
Vichache huvichagua, vya haraka kuchanua,
Mkazo akatilia, kazi viweze fanziwa,
Hivyo vikishakua, vingi sana huvizaa,
Kiongozi wa ukweli, hatojishibisha kwanza:
Huwashibisha raia.
Watu wake huwajua, sio kuwasingizia,
Ugomvi wetu ni njaa, malau pia balaa,
Na dharau za mkaa, mweupe zisizofdaa,
Kiongozi wa ukweli, hatojishibisha kwanza:
Huwashibisha raia.
Kama vile motokaa, gia zake hutambua,
Ya kwanza ikishaingia, zingine zinafatia,
Ndivyo ilivyo dunia, yapo ya kutangulia,
Kiongozi wa ukweli, hatojishibisha kwanza:
Huwashibisha raia.
Halisi ninatambua, lipo hili lenye njaa,
Bei ukizitanzua, maisha nafuu huwa,
Wala si kujisifia, milioni wafulia,
Kiongozi wa ukweli, hatojishibisha kwanza:
Huwashibisha raia.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment