Sunday, November 18, 2012

Zanzibar bado lulu



SABABU haitokuwa, madaraka kuatiwa,

Yake ikayaamua, yawezayo kuifaa,

Vingine inapokuwa, utumwa utarejea,

Kama nchi Zanzibar, yastahili kuamua!



Pacha wanatambuliwa, muungano kuridhia,

Ila bado ni jamaa, tofauti inakuwa,

Bara yao familia, kadhalika Zanzibar,

Kama nchi Zanzibar, yastahili kuamua!



Kila mtu anajua, wadini hatujakuwa,

Kiwacho ni yetu njaa, chakula tunafulia,

Si uongo nawambia, hali yetu naijua,

Kama nchi Zanzibar, yastahili kuamua!



Vyovyote waweza kuwa, bara wanavyoamua,

Ila sisi twajijua, Islamu twajaliwa,

Vingine haitakuwa, hadi mwisho wa dunia,

Kama nchi Zanzibar, yastahili kuamua!



Dini wanaoichafua, nyie mmewaridhia,

Dawa yenu kuwatoa, tawba tukaivua,

Kesi kutotuachia, kwa ubaya kuanzia,

Kama nchi Zanzibar, yastahili kuamua!



Usaliti haijawa, kutaka jitegemea,

Kama ndio ingekuwa, kusingekuwa na ndoa,

Watoto wakazuiwa, kwa nyumbani tu kukaa,

Kama nchi Zanzibar, yastahili kuamua!



Ni nzuri hii nia, nchi kujitegemea,

Yake ukiyaamua, tasihili kwendlea,

La keshokutwa likawa, hivi leo latokea,

Kama nchi Zanzibar, yastahili kuamua!



Mkoa haitakuwa, nchi huru tunajua,

Katiba inaridhia, malezi kujifanzia,

Mipango ikaibua, nchi ikainyanyua,

Kama nchi Zanzibar, yastahili kuamua!



Viko vidogo visiwa, ubora vimejaliwa,

Seychelles wanapaa, sisi tunaogelea,

Mbeleko kutoitoa, kisiasa ni udhia,

Kama nchi Zanzibar, yastahili kuamua!



Jana tungeliamua, kuuza na kununua,

Ndio kazi kubwa kuwa, Afrika kutufaa,

Fursa tunachezea, twangoja kusaidiwa ?

Kama nchi Zanzibar, yastahili kuamua!



Sadaka tunachukua, wazima tuliokuwa,

Dini hili lakataa, jasho budi kulitoa,

Fikirini maridhia, ujinga msioujua,

Kama nchi Zanzibar, yastahili kuamua!



Macau waendelea, sisi nyuma twabakia,

Singapore nayo pia, nusu hawajafikia,

Baraka twazichezea, kw autoto kujitia,

Kama nchi Zanzibar, yastahili kuamua!



Wakubwa tumeshakua, bara kuisadiia,

Na mojawapo ya njia, ni uhuru kuamua,

Yetu tukajifanyia, pande zote kutufaa,

Kama nchi Zanzibar, yastahili kuamua!



Zanzibar iling'aa, mwanga bara kuingia,

Leo gizani twakaa, yatutania dunia,

Amkeni Wazanzibar, Afrika kuifaa,

Kama nchi Zanzibar, yastahili kuamua!



Dubai kuifikia, sio kazi itakuwa,

Ila tukishaamua, mambo kujiandalia,

Pawe kweli na ubia, wa nchi kuinyanyua,

Kama nchi Zanzibar, yastahili kuamua!



Sauti watasikia, wa Mrima walokuwa,

Zikaingia bidhaa, kwenda kote kusambaa,

Bei rahisi ikiwa, nasi juu tutakuwa,

Kama nchi Zanzibar, yastahili kuamua!



Kiwanja kukipanua, kimataifa kikawa,

Mithili Dubai kuwa,ndege kwa wingi kutua,

Kubwa zilizokuwa, vikubwa kuvinyanyua,

Kama nchi Zanzibar, yastahili kuamua!



Bandari kuitanua, manowari kuingia,

Na meli za abiria, malefu kutuletea,

Nchini kuja tumia, hazina yetu kujaa,

Na meli za abiria, maelfu kuingia,



Viwanja vinatakiwa, kukimbia motokaa,

Hiyo moja Formula, kwa Pemba pia Unguja,

Mashindano kwandaa, wageni tele kujaa,

Kama nchi Zanzibar, yastahili kuamua!



Golfuu inatakiwa, upya kuifufua,

Viwanja tulivyoua, basi vipya kuzaliwa,

Ni mchezo maridhia, waucheza bilionea,

Kama nchi Zanzibar, yastahili kuamua!



Viwili vyaweza kuwa, kwa Pemba na Zanzibar,

Sayakati kuingia, tuitingishe dunia,

Golfu ikasaidia, umaskini kuutoa,

Kama nchi Zanzibar, yastahili kuamua!



Utalii watakiwa, wa wananchi ukawa,

Msaada kupatiwa, ya kwao kujifanyia,

Vibanda kujijengea, na hadhi vilivyokuwa,

Kama nchi Zanzibar, yastahili kuamua!



Watalii wafurahia, nyumbani kuja kukaa,

Na wa jamii ukiwa, mgahawa utafaa,

Asili kujionea, na utamaduni pia,

Kama nchi Zanzibar, yastahili kuamua!



Hili wanalokataa, uchumi wanafulia,

Wanashindwa kuelewa, inakokwenda dunia,

Aproni wang'ang'ania, kitu isiyowafaa,

Kama nchi Zanzibar, yastahili kuamua!





Mola umenisikia, nilipoiomba dunia,

Zanzibar kujalia, ipate kuendelea,

Kwa yake kuyaamua, bara ikisaidia,

Kama nchi Zanzibar, yastahili kuamua!



Watu kuwazidishia, dhiki zipate pungua,

Maisha yatuonea, furaha inakimbia,

Nawe unajionea, na ukweli waujua,

Kama nchi Zanzibar, yastahili kuamua!



Sadaka ninaitoa, shairi kuwatungia,

Baraka lazingojea, ili kazi kufanziwa,

Kama zana kuja kuwa, nchi ipate jaliwa,

Kama nchi Zanzibar, yastahili kuamua!



Zanzibar

Novemba 14, 2012











No comments: