Wednesday, November 14, 2012

Mwonewa akigeuka


Akija kuwa mwonea, kwa aliyekionewa,

Kisasi akakitia, mtima kuutumbua,

Huwa fukwe zaambaa, baharini kuingia,

Mwonewa akigeuka, akaja kuwa mwonea !



Maji ardhi huvaa, pwani yote kutembea,

Mradi ukauzua, wa damu kwenda jitoa,

Ya siri usiyojua, dhahiri yakatokea,

Mwonewa akigeuka, akaja kuwa mwonea !



Mwili hawajaujua, ni mmoja ulokuwa,

Ule ukiuonea, wako nao waumia,

Na hili halijakuwa, ila kwa waliojaliwa,

Mwonewa akigeuka, akaja kuwa mwonea !



Viumbe wote wamoya, vingine haijawa,

Kizazi kilozaliwa, asili twaitambua,

Vipi jino kujitoa, uchungu kutosikia ?

Mwonewa akigeuka, akaja kuwa mwonea !



Wewe unalofurahia, mwenzi alihitajia,

Majivuno ni udhia, tena mkubwa balaa,

Vya msingi vyatakiwa, kila mtu kuambua,

Mwonewa akigeuka, akaja kuwa mwonea !



Vitu wanaoringia, umoja wanauua,

Ndipo huja kuzaliwa, tamaa waliojaa,

Elfu kuiridhia, hata mtu kumuua,

Mwonewa akigeuka, akaja kuwa mwonea !



Roho zao huziua, utu wakaufikia,

Vigumu kutambua, na heri yasiyokuwa,

Ubayani kubakia, hadi roho kutolewa,

Mwonewa akigeuka, akaja kuwa mwonea !





No comments: