Thursday, November 8, 2012

WAFIKIRIE WAJUKUU

Nani utamuachia, wajukuu kwangalia,


Fisadi waliokuwa, huruma wasiokuwa,

Au mtu katokea, wa kuweza aminiwa?

Fikiri ya wajukuu, kabla kununuliwa!



Wana wakuangalia, nini utachoamua,

Nawewe kununuliwa, au fedha kukataa,

Adili kuichagua, uokoe Tanzania?

Fikiri ya wajukuu, kabla kununuliwa!



Utume sijaupewa, ni raia wanambia,

Mshairi wanijua, kutumwa sintokataa,

Lao ndani nalitia, nyie kulifikiria,

Fikiri ya wajukuu, kabla kununuliwa!



Mjumbe nimeambiwa, haya kuyaulizia,

Hatima waihofia, kesho yao kuwa baa,

Nanyi mtaloamua, ndilo huonesha njia,

Fikiri ya wajukuu, kabla kununuliwa!



Kutumwa si kukataa, kazi nimeiridhia,

Chumvi sintaongezea, wala sukari kutia,

Mizani sasa isawa, mnaweza kuamua,

Fikiri ya wajukuu, kabla kununuliwa!



Amueni la ulua, adili lililojaa,

Wepesi litalotia, chama kikakubaliwa,

Kisionekane balaa, mumiani kimekua,

Fikiri ya wajukuu, kabla kununuliwa!



Wote ninawatambua, nchi mmetumikia,

Na wengine twawajua, njia walizopitia,

Mkato una udhia, tena ni kubwa nazaa,

Fikiri ya wajukuu, kabla kununuliwa!



Kunguru ana tabia, uoga ukimwingia,

Bawa akalikimbia, adui kumdhania,

Waliojihesabia, watakiwa kujitoa,

Fikiri ya wajukuu, kabla kununuliwa!



Vingine haitakuwa, heshima itapotea,

Na wanaong'ang'ania, wanapaswa kulijua,

Haya sijajisemea, ni ujumbe mwatumiwa,

Fikiri ya wajukuu, kabla kununuliwa!



No comments: