Sunday, November 18, 2012

MIZIZI JABALINI

MBEGU wamezitupia, katika mawe kuota,


Miye nimeangalia, na ugumba kuusuta,

Kama vile ni ruia, bado ningali naota,

Mizizi katika mawe, mmea hauachi kufa !



Yao walikimbilia, na wakanipita puta,

Nyuma hawakuangalia, ya mbele wakiyafata,

Chini hawakuangalia, niendapo waokota,

Mizizi katika mawe, mmea hauachi kufa !



Wafata historia, inayozidi wasuta,

Yamebakia mazoea, umeanguka ukuta,

Nao wanaegemea, huku wangali watweta,

Mizizi katika mawe, mmea hauachi kufa !



Mambo wameyapangua, wabaki cheza karata,

Kesho inawachachia, wanatifua matuta,

Vyanzo wanakovijua, sasa ufuta wateta,

Mizizi katika mawe, mmea hauachi kufa !



Hali ninaihofia, inanukia matata,

Mwanzo itapaanzia, kuongezeka ukata,

Watu wakajinunua, acha wa kununuliwa,

Mizizi katika mawe, mmea hauachi kufa !



Mbata wataziangua, na miembe kupukuta,

Na mbichi zilizokuwa, moto ziende kuota,

Hali ikishafikia, watalitwanga pepeta,

Mizizi katika mawe, mmea hauachi kufa !



Mizizi mkitifua, mtake tena kuota,

Ardhi huikataa, vya chini vikatokota,

Chinichini kutambaa, juu yashindwe kupita,

Mizizi katika mawe, mmea hauachi kufa !



Mkikota mimea, na watu kuwaokota,

Lipi la kujipandia, hadi hadhi kuipata,

Miaka itaamua, yaishe ya kumetameta,

Mizizi katika mawe, mmea hauachi kufa !



Mti hauwezi kua, wala tunda kulipata,

Mizizi ikijifia, huwa vigumu kuota,

Taratibu hujifia,ikabakia kutweta,

Mizizi katika mawe, mmea hauachi kufa !



Mliyoyakimbilia, ikawa sasa kunyata,

Na kilichowazuzua, kikabakia kiota,

Mahame yakabakia, na njia zilizotota,

Mizizi katika mawe, mmea hauachi kufa !

No comments: