Thursday, November 8, 2012

Rushwa kwisha haiwezi

WAKUU wakiamua, chamani kutoridhiwa,

Tutaipiga hatua, usafi ukarejea,

Haya tukivumilia, naona twenda pabaya,

Rushwa kwisha haiwezi, ila yaweza pungua !

Uchina yanatokea, na watu wanauawa,

Chama kimekazania, chamani kutoachiwa,

Ole wako 'kigunduliwa, risasi ni yako dawa,

Rushwa kwisha haiwezi, ila yaweza pungua !

Chama chajifaragua, serikali kutokuwa,

Mangimeza kwangaliwa, wasije wakapotea,

Udhibiti watimia, kila siku wafichua,

Rushwa kwisha haiwezi, ila yaweza pungua !

Usafi hadhi hutia, chama kutodharauliwa,

Haya ukiyakataa, juu sana kitakuwa,

Vinginevyo 'kiachiwa, kusambaratika kwawa,

Rushwa kwisha haiwezi, ila yaweza pungua !

Yafaa kujiangalia, binafsi tulokuwa,

Mzigo tukishakuwa, mapema kujichomoa,

Ni vizuri kujifia, ili chama kwendelea,

Rushwa kwisha haiwezi, ila yaweza pungua !

Sasa tuking'ang'ania, riziki haitakuwa,

Makubwa nayahofia, chama kuja kusumbua,

Si safi hali ya hewa, kwa mashine twapumua,

Rushwa kwisha haiwezi, ila yaweza pungua !

Ukiongeza na njaa, nchi inayosumbua,

Wahasirika jamaa, baya watavumiia?

Mikono wakinyanyua, nani atayeumia?

Rushwa kwisha haiwezi, ila yaweza pungua !

No comments: