Thursday, November 8, 2012

Wachiani Tanzania




SIULIZE uwe nani, siku haujazijua,

La faragha hilo mbwani, ughaibuni waingia,

Janibu umashakani, yaweje usiyoyajua ?

Wachiani Tanzania, hivi leo 'kiondoka?



Yaweje ughaibuni, sote tunakoelekea?

Kakupa nani mizani, mwenyewe kujipimia,

Yakukimbiaje soni, na haya kutojionea,

Wachiani Tanzania, hivi leo 'kiondoka?



Mkono wa kiunoni, nani ameuachia,

Wajua wanazuoni, wengi wasichokijua,

Unavyozama nuruni, ndivyo giza lazidia,

Wachiani Tanzania, hivi leo 'kiondoka?



Mapema huwa yamini, yafaa kuiamua,

Tanzania wachiani, wana waje kumbukia,

Wakawepo hesabuni, siku ya kuhesabiwa ?



Nini ulichobaini, au wewe kuzindua,

Kikawa nayo thamani, watu wetu kuwafaa,

Wakukumbuke miakani, muasisi ulikuwa,

Wachiani Tanzania, hivi leo 'kiondoka?



Pia nao masikini, yako wakajivunia,

Kwa kuwapa afueni, nafuu kujionea,

Wasiwe tena shakani, riziki kujipatia,

Wachiani Tanzania, hivi leo 'kiondoka?



Wanaoishi gizani, nuruni wakaingia,

Maji wapatao topeni, bombani wakapatiwa,

Afya kutoihini, maisha kufurahia,

Wachiani Tanzania, hivi leo 'kiondoka?



Waishio maanyatani, nyumba wakajipatia,

Wakaongeza thamani, kwa mema kuyaringia,

Wawe na matumaini, mengi kujitafutia,

Wachiani Tanzania, hivi leo 'kiondoka?



Wapiga vita uduni, au ukubwa ni njaa ?

Nini yako madhumuni, kama si watu kwendelea?

Nani unamthamini, kama siye Mtanzania?

Wachiani Tanzania, hivi leo 'kiondoka?









No comments: