Wednesday, November 28, 2012

Bibi msikilizeni


HEBU kitako kaeni, muwasikize wazee,
Hali zao taabani, nani wakamlillie,
Mwamsubiria nani, ya kwao awafanyie ?
Bibi msikilizeni, ana lake la kusema.

Bibi msikilizeni, na babu mkaongee,
Watu hawa si wageni, ndiko huko mtokee,
Muitunge afueni, kitaifa kuwafaa,
Bibi msikilizeni, ana lake la kusema.

Yao ni bure thamani, si ya kuwashinda nyie,
Ila muda hamuuoni, yao myafikitie,
Wanalilia vijijini, wazima mhurumie,
Bibi msikilizeni, ana lake la kusema.

Mia mbili ni hisani, kuipata ni ndotowe,
Wauliza nchi gani, yawa myaongozaye,
Mwawasemea kina nani, hadi leo mjisisfie?
Bibi msikilizeni, ana lake la kusema.

Maji hayapatikani,hadi mtu utembee,
Kilomita za uzani, na mzigo uchukuwe,
Inawavia imani, kwa maneno msiwapepee,
Bibi msikilizeni, ana lake la kusema.

Chakula chao utani, kwa njaa wajishibie,
Au mboga mgagani, maporini kuwafae,
Na majoka wa mwituni, hapo wasiwazuie,
Bibi msikilizeni, ana lake la kusema.

Uswizi zichukeni, vijiji zikawafae,
Huu ni unyama gani, kimya mjitangazie,
Hali kwamba vijijini, kizazi wakijutie ?
Bibi msikilizeni, ana lake la kusema.

Balaa tuepukeni, kwa kuwafaa wazee,
Tusiwe ni hayawani, sikuzote tulaaniwe,
Jitazameni moyoni, nchi isiwapotee,
Bibi msikilizeni, ana lake la kusema.

No comments: