Sunday, November 18, 2012

Halali na haramu

YA halali na haramu, viumbe mmeumbiwa,

Mkapewa na fahamu, tofauti kuijua,

Kafiri na Islamu, wote hili walijua,

Mwatakiwa kuyajua, ya halali na haramu !

Kukumbusha yangu zamu, wote mnaofatia,

Nisiwe wa kudhulumu, kuwa hili sikwambia,

Nalijua, situhumu, ukweli nauridhia,

Mwatakiwa kuyajua, ya halali na haramu !

Kumbukeni Jahanamu, muweze kuikimbia,

Mkijitia muhimu, na hili kutohofia,

Maisha ni madhulumu, huruma hayajapewa,

Mwatakiwa kuyajua, ya halali na haramu !

Yakuuliza kalamu, miaka ulivyotumia,

Kama una elimu, hesabu utadaiwa,

Na ujana wa hanjamu, kizaazaa huzua,

Mwatakiwa kuyajua, ya halali na haramu !

Mali ukitakadamu, nayo itauliziwa,

Na cheo ukikihimu, kuna deni wadaiwa,

Mchungi huna utamu, hadi hesabu kuijua,

Mwatakiwa kuyajua, ya halali na haramu !

Niepushe na haramu, halali kunijalia,

Nakuomba Mukadamu, dua yangu kusikia,

Sijaliwi ufahamu, ila unaonijalia,

Mwatakiwa kuyajua, ya halali na haramu !

No comments: