Thursday, November 8, 2012

Refa rafu akianza

JARIBU kufikiria, mechi inaendelea,

Kisha refa kaamua, yeye ndiye kuanzia,

Pande zote kabutua, na viatu kuwatia,

Refa rafu akianza, uwanja vipi 'takuwa ?

Urefa akaamua, pekee yeye akawa,

Wasaidizi kapewa, yeye amewakataa,

Lao ameligomea, hataki kulikisikia,

Refa rafu akianza, uwanja vipi 'takuwa ?

Watu wanamuhofia, kaingia ukichaa,

Au ameishapagawa, mke amemkimbia?

Au nzaiko imekoa, mwenyewe kumuingia?

Refa rafu akianza, uwanja vipi 'takuwa ?

Kadi ovyo anatoa, wachezaji wapungua,

Na sasa wamebakia, wachache wasotimia,

Mashabiki wazomea, hivi sasa ni udhia,

Refa rafu akianza, uwanja vipi 'takuwa ?

Mechi yataka nasaha, na vingi kuvumilia,

Haraka ukiamua, utamu wote hupaa,

Shubiti ikabakia, na mawe kukufatia,

Refa rafu akianza, uwanja vipi 'takuwa ?

Misongo isipoachiwa, mafuu huambulia,

Wengi kuchanganyikiwa, mengine wakaamua,

Kimya ukikisikia, mshindo utatokea,

Refa rafu akianza, uwanja vipi 'takuwa ?

Uwanja wakiumbia, wapi utawaonea,

Na vipi utalijua, watakalojisukia,

Mke gunia huvaa, mme gauni kuvaa,

Refa rafu akianza, uwanja vipi 'takuwa ?

Cheichei naitoa, kwa ndgu nao jamaa,

Mwana ameshambiwa, kuzika imebakia,

Nguu mlima haijawa, safari sasa upya,

Refa rafu akianza, uwanja vipi 'takuwa ?

No comments: