Sunday, November 18, 2012
Wajumbe tena hatuna
Wajumbe tumepoteza, watumwa wanabakia,
Viumbe wakujiuza, mfukoni wametiwa,
Kwa sasa ni kama viza, yai lisilotufaa,
Sasa tunao watumwa, wajumbe tena h atuna !
Wajumbe wachiuza, uwakilishi kuua,
Nchi tunaipoteza, kama nguo kuivua,
Uchi kujitembeza, ikatucheka dunia,
Sasa tunao watumwa, wajumbe tena h atuna !
Kazi wanaoongoza, wanasiasa Tanzania,
Vyama bila kutangaza, hakuna asiyejua,
Ujumbe sasa kujiuza, na kura ikanunuliwa,
Sasa tunao watumwa, wajumbe tena hatuna !
Dini ilishapoteza, udini wakataliwa,
Ila roho wanauza, kuizuia dunia,
Wadhania waongoza, kumbe wanaangamia,
Sasa tunao watumwa, wajumbe tena h atuna !
Ni samaki wameoza, kwenye tenga walojaa,
Vikundi wanavyokuza, vya njaa kujigangia,
Fedha wanatanguliza, Nyerere alohofia,
Sasa tunao watumwa, wajumbe tena h atuna !
Siasa waendeleza, ufukara kuulea,
Wao wanavyoangaza, utumwa wasaidia,
Njaa watu ikiliza,mkubwa unabakia,
Sasa tunao watumwa, wajumbe tena h atuna !
Hawataki kuongoza, umaskini kutoa,
Wajua haya wakifanza, uhutu twajipatia,
Na kuringa tutaanza, kurani kuwakataa,
Sasa tunao watumwa, wajumbe tena h atuna !
Hivyo wanang'ang'aniza, ufukara kubakia,
Kwao ngao wanatunza, ukubwa kutopotea,
Ajabu ya muujiza, na ibra ya dunia,
Sasa tunao watumwa, wajumbe tena h atuna !
Heshima waipoteza, wao wanajisifia,
Hata watoto wajuza, ni kicheko imekuwa,
Baba na mama kutunzwa, ardhi wakaiachia ?
Sasa tunao watumwa, wajumbe tena h atuna !
Na tena wanachotunzwa, ni chache zao rupia,
Thamani zimepoteza, kitu hazitosaida,
Laiti wangejitunza, tajiri wangelikuwa,
Sasa tunao watumwa, wajumbe tena h atuna !
Mazoe kumbe kuoza, wachache wanaojua,
Kila unapoangaza, hali ukakubalia,
Kumbe juu ungeweza, aliye akuzuia,
Sasa tunao watumwa, wajumbe tena h atuna !
Akili wanakuteza, na mitego kukwekea,
Wajua hujui tunza, wala kujitafutia,
Hivyo wanakulemaza, waweze kukutumia,
Sasa tunao watumwa, wajumbe tena h atuna !
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment