Barri ni mwenye kujua, hata tusiyoyajua,
Na anapotangulia, wasiwasi hututoa,
Tusijifanye twajua, chicha tukaambulia,
Ni mwepesi wa kupanga, huwezi shindana naye !
Asili tunaijua, twakubali nunuliwa,
Mfukoni tukatiwa, ya wengine kuriddhia,
Hali fika tunajua, twaweza jitegemea ?
Ni mwepesi wa kupanga, huwezi shindana naye !
Yetu tukijipangia, mbele budi kusogea,
Kuna ndugu wangojea, mkono kutupatia,
Vigumu haitakuwa, dini yetu waijua,
Ni mwepesi wa kupanga, huwezi shindana naye !
Hadithi zasimuliwa, bara yaliyotokea,
Jerumani kashupaa, udini kuutambua,
Hisabu wakachafua, ili kwenda waridhia,
Ni mwepesi wa kupanga, huwezi shindana naye !
Ndio kisa kukataa, ubaya lisilokuwa,
Mbona leo twasikia, Marikani waridhia,
Kura walipojipigia, dini siri haikuwa,
Ni mwepesi wa kupanga, huwezi shindana naye !
Ujanja wakitumia, pabaya wanatutia,
Wajifanyao kujua, ikawacheza dunia,
Aibu yawaingia, hadi nje wahofia ?
Ni mwepesi wa kupanga, huwezi shindana naye !
Data kaziye kuzaa, yote nje kuanikwa,
Vingine haijakuwa, uongo unapotia,
Kazi hazitowafaa, hubakia kuchezewa,
Ni mwepesi wa kupanga, huwezi shindana naye !
Takwimu zakuchambua, kisha zikabanguliwa,
Zinakuwa na udhia, kupikwa huja kataa,
Chunguni kinachotiwa, kibichi kikabakia,
Ni mwepesi wa kupanga, huwezi shindana naye !
Sunday, November 18, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment