Sunday, November 18, 2012

Aali wastahili



Akili zikifulia, madoho huyaridhia,

Mbali hautoyajua, wala hutojionea,

Yako ukayadhania, ni makubwa yamekuwa,

Aali wastahili, tumeangusha wananchi !



Yetu ukiangalia, sisi nyuma twabakia,

Sote tulipoanzia, sawasawa ilikuwa,

Kundi ukilichukua, twadorora Tanzania,

Aali wastahili, tumeangusha wananchi !



Ni bure kujisifia, kwa ukweli lisokuwa,

Ili wende hurumiwa, wembe ukiandaliwa,

Kinyozi hajajinyoa, naye huomba nyolewa,

Aali wastahili, tumeangusha wananchi !



Ila walioingia, mashine wanatumia,

Hiyo hiyo hutumia, na wao wakajinyoa,

Kisha wakatuzingua, na hasira kututia,

Aali wastahili, tumeangusha wananchi !



Mengine ni kunyamaa, sauti kutotoa,

Chumvi ukizidishia, chakula hakitaliwa,

Kwanza mngeliyajua, uzito kujipimia,

Aali wastahili, tumeangusha wananchi !



Pande mkaangalia, ni wapi imezidia,

Kama kwenu imekua, hayao yenu manufaa,

Wengine huangalia, kama wana manufaa,

Aali wastahili, tumeangusha wananchi !



Kitu wasipoambua, vipi watakusifia,

Mtu bora kujijua, na hadhara kuijua,

Wapo wa kushangilia, kwa malipo kugaiwa,

Aali wastahili, tumeangusha wananchi !







Umasikini uchafu



Sio la kuliringia, hili linapotokea,

Ni aibu hututia, na wengine kukimbia,

Haya ikawaingia, wote wanaojijua,

Umasikini uchafu, unafaa kufagiwa!



Nchi hutia madoa, na mabaka kuzagaa,

Watu yakawaumbua, kila walipotulia,

Mgeni kuwa udhia, haya akijionea,

Umasikini uchafu, unafaa kufagiwa!



Vya msingi vyatakiwa, waziri kutuambia,

Kwanini tunafulia, haviwezi tengamaa,

Ni ishara za balaa, wageni wazihofia,

Umasikini uchafu, unafaa kufagiwa!



Nchi isiyo maua, nani kuitembelea,

Kwa maji tunafulia, wapi yanakopitia,

Bustani zaugua, bima hazikujaliwa,

Umasikini uchafu, unafaa kufagiwa!



Nchi haina kung'aa, nani kuifurahia,

Ni vichaka imekua, na dampo ni majaliwa,

Mvuto unapotea, kipi cha kujionea ?

Umasikini uchafu, unafaa kufagiwa!



Ya msingi yatakiwa, kufanya Watanzania,

Na nyie wa kutembea, mnaoingia Ulaya,

Nchi mmejionea, usafi zinavyokuwa,

Umasikini uchafu, unafaa kufagiwa!



Mbona kwetu ni kinyaa, h ata tunajichukia,

Hili kweli latakiwa, nalo likasaidiwa,

Au kujipanga waa, na mwanawe ndiye jaa ?

Umasikini uchafu, unafaa kufagiwa!





No comments: