Thursday, November 8, 2012

WAJA WAENDESHA UTUMWA


NYUMA ukiangalia, picha ya historia,

Wachuuzi walokuwa, watumwa kuwanunua,

Ndio leo wanunua, vijana kuwatumia,

Waendesha utumwa, hao wote wangekuwa;

Kazi watu kununua!



Tofauti haijawa, wala h aitatokea,

Miaka yajichambua, hali sawa inakuwa,

Tumbo anayejaliwa, hajui kulitumia,

Waendesha utumwa, hao wote wangekuwa;

Kazi watu kununua!



Hajui kulitumia, ila watu kununua,

Kisa chake kuhofia, chakula kuja pungua,

Ya kesho ajiandaa, ya leo akafulia,

Waendesha utumwa, hao wote wangekuwa;

Kazi watu kununua!



Huwa amenunuliwa, na njaa anayemzidia,

Lengo keshajiandikia, utajiri wa dunia,

Kichochoro atumia, kwenda 'nakojiendea,

Waendesha utumwa, hao wote wangekuwa;

Kazi watu kununua!



Na wote wasiojijua, kwalo hili hupagawa,

Kama vipofu wakawa, jengine kutojionea,

Na uziwi huingia, la mtu kutosikia,

Waendesha utumwa, hao wote wangekuwa;

Kazi watu kununua!







No comments: