Wednesday, November 14, 2012

Sharabaro mil'onea

sikukNajifunika ruia, mchana kujiotea,

Utajiri kuuvua, kama samaki wa jua,

Au nyota zilizokuwa, zaanguka na mvua,

Sharobaro mil'onea, njozi ninajiotea.



Kitini nilipokaa, fedha ninajioinea,

Na nyingine zina mbawa, juu sasa zinapaa,

Machoni zikaingia, moyoni zikatokea,

Sharobaro mil'onea, njozi ninajiotea.



Mtoni zimetulia, kitandani nikikaa,

Habiba nashikilia, siwezi kuuachia,

Huyu wangu maridhia, tunu niliyojaliwa,

Sharobaro mil'onea, njozi ninajiotea.



Pumzini husikia, fedha ninahesabiwa,

Malaika kaajiriwa, mwana wa hii dunia,

Sauti wimbo ikawa, usingizi kunitia,

Sharobaro mil'onea, njozi ninajiotea.



Ya wengine kusifia, hiyo ni yangu tabia,

Mwenyewe wa kulegea, kushindwa na kukataa,

Yangu kujisimamia, naona ninachezewa,

Sharobaro mil'onea, njozi ninajiotea.



Uzuri nashangilia, kitu usionifaa,

Koo kujikaukia, bila ya maji kupewa,

Na chakula ni mzaha, mwana asichoshibia,

Sharobaro mil'onea, njozi ninajiotea.



Naitazama dunia, mlipaji kwenye riha,

Ndio alokusudiwa, ni nani wa kunifaa,

Siku nitakapojijua, mbali sana kukimbia,

Sharobaro mil'onea, njozi ninajiotea.



Ni marashi nanukia, kila nikijisikia,

Thamani yaliyokuwa, nchini hayajaingia,

Ikawa yangu hadaa, sinuki, nitanukia,

Sharobaro mil'onea, njozi ninajiotea.



Sinuki, nitanukia, hata roho kitolewa,

Utume kujidhania, hadimu niliyekuwa,

Hadi ninapoambiwa, ninaingia kubaya,

Sharobaro mil'onea, njozi ninajiotea.

No comments: