Wednesday, November 14, 2012

Sera za Watanzania

Nani kalifikiria, na chama kukigawia,

Iweje sera ikawa, chama inazinunua,

Na sote twatarajia,, kwa yake tukajaliwa,

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Labda rushwa kutoa, hiyo ya kwao twajua,

Ufukara kuzidia, ndipo hapa tumekaa,

Na upofu kujitia, kitu halijasaidia,

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Kwa uziwi kusifiwa, haya tungeishajua,

Ya msingi yamejaa, kufanza tunatakiwa,

Hapo tukishafikia, sera twaweza ibua,

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Nani amekuambia, kwenye hii Tanzania,

Kuna watu wakataa, kilimo kutuhudumia,

Na vyama tumevizua, chakula kutotumia ?

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Nani amekuambiwa, kunao Watanzania,

Gizani waazimia, sikuzote watakaa,

Vijinga wakatumia, mwangaza kujipatia,

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Na eti wa kuwatoa, budi mchama akawa ?

Kama mtu hujifia, hicho cha kutegemewa ?

Na mumiani kikiwa, ndio hofu kinatia,

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Nani amekuambia, chama fedha kimejaa,

Wapi kinajipatia, kama si hazina pia,

Kingi wakakumbatia, kidogo wakaachia,

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Serikali kuzifua, lazima inatakiwa,

Leo moja ukavaa, kesho nyingine kutwaa,

Nguo moja kitumia, fukara utadhaniwa,

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Serikali ni kuvaa, na kisha ukaivua,

Unapoing'ang'ania, inazidi kuchakaa,

Uzuri haitakuwa, ikianza kufubaa,

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Jana kijani kutia, leo bluu watumia,

Rangi nyingi zimejaa, moja tu unachagua,

Kuna zingine balaa, bahati hukukimbia,

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Nani amekuambia, njia wanazikimbia,

Wazihofu Tanzania, kuwaletea mabaa,

Maporini wapitia, salama kujisikia?

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Sera ni kama bidhaa, vitu hivyo hutumiwa,

Vitu vinapomfaa, kila mtu hutumia,

Ila kama vya rushuwa, muumini hukataa,

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Sera kama vile hewa, kila mtu hupumua,

Mazuri kuyachagua, binadamu ni tabia,

Hawezi akaparamia, baya yeye kuchagua,

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Nani amekuambia, elimu haitatufaa,

Hivyo wajinga wang'aa, elimu kuitania,

Na mikopo kuzuia, wenetu kutowafaa?

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Nani amekuambia, ataka lima kinjaa,

Pamba akijivunia, soko kutotengenea,

Akasikiza umbeya, na hadithi kupigiwa ?

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Nani amekuambia, afya ni kitu balaa,

Huduma bure kutoa, watu wengi wahofia,

Ila ujira wa njaa, ukawa wapalilia,

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Ila ujira wa njaa, ukawa wapalilia,

Dau wakalizindua, sasa milioni kuwa,

Senti zikishapungua, huondoka wako dia,

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Nani amekuambia, eti nyumba twakataa,

Manyata twakumbatia, na porini kutulia,

Mjini twakuhofia, hatutaki kwendelea,

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Kama sio yenu nia, fahari kujionea,

Neema kujisikia, nyie mliojaliwa,

Vyote kuwatiririkia, wote mliobarikiwa,

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Siri wameigundua, mwahofu kukataliwa,

Binti ukimjengea, aweza nje kukutoa,

Mwingine kukubaliwa, na kitu asiyekuwa,

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Kwenu ni Watanzania, wanajua kuchagua,

Nyumba wakijipatia, wengine watachangua,

Uhuru kujipatia,, hamwezikuwaswagia,

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Nani amekuambia, wageni ndio wafaa,

Kukopa tukijazia, mabenkini zikajaa,

Ila akiwa mzawa, shuruti anaekewa ?

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Nani amekuambia, hatutakiwi Ulaya,

Pasi mkazizuia, wenyeji kujipatia,

Ila wa Somalia, raia wao wakawa ?

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Nani amekuambia, juujuu ukijua,

Mweledi umeshakua, bila ya kuyachunua,

Ng'ombe wayo huuziwa,mjini ukaingia,

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Nani amekuambia, hisa tumeshazikataa,

Ila palipo udhia, utani pia mzaha,

Oksijeni kwishiwa, bado najiulizia ?

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Nani amekuambia, madini yamilikiwa,

Na wachache walokuwa, matofali wakapewa,

Nani anayetumia, ujira akishapewa ?

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Langu ninamalizia, kwa uchama kukataa,

Mengi yanayotakiwa, hayo ya wote yakawa,

Programu kuridhia, nchini kufumuliwa,

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

Serikali ya pamoya, akili iliyojaa,

Hiyo nitafurahia, na sio ya kutumiwa,

Uhuru iliyokuwa, yake inayaamua,

Sera za Watanzania, hakuna sera ya chama:

Hasa vya msingi vikiwa !

No comments: