Wednesday, November 14, 2012

Ilikuwa ni usiku




Unaondoka usiku, afajiri yajongea,

Kikoi chake kihuku, jogoo kakifatia,

Apate amsha kuku, sala inakaribia,

Ilikuwa ni usiku, asubuhi sasa yaja!



Maisha ya panya buku, chini chini kuingia,

Mialiko ni ruzuku, riziki kuongezewa,

Iliyokuwa na luku, wengine wanafulia,

Ilikuwa ni usiku, asubuhi sasa yaja!



Vitendo ni marufuku, kutendewa ya kufaa,

Ila kuchinjiwa kuku, ule ulewe hadaa,

Kisha ukapigwa chuku, pembeni kwenda ngojea,

Ilikuwa ni usiku, asubuhi sasa yaja!



Tumekicheza kiduku, kwa ngapi tumesogea,

Hatua zenye udaku, vitamu kuambulia ?

Hatutaishi kwa buku, hata mia zingekuwa,

Ilikuwa ni usiku, asubuhi sasa yaja!



Ukigeuzwa kasuku, lingine hautojua,

Utabakia uchaku, chakubanga kumfaa,

Ukabaki pekupeku, uzee ukishaingia,

Ilikuwa ni usiku, asubuhi sasa yaja!



Ya kwenu hayako huku, bali mlikokalia,

Nalo msipolishuku, mtazidi kuchezewa,

Chini mkabaki huku, wao juu wakapaa,

Ilikuwa ni usiku, asubuhi sasa yaja!





No comments: