Wednesday, November 28, 2012

Huu wote hautoshi

Majeta tumejaliwa, viumbe wasioshiba,
Chote hujilimbikia, na njaa bado huwakaba,
Dunia hawajajua, watia kwenye viroba,
Huo wote hautoshi, wape nchi watashiba ?

Maneno wamuachia, ila vitendo ni haba,
Mgongo wamridhia, wajifiche kwazo toba,
Na nuksi na balaa, kisima chao chabeba,
Huo wote hautoshi, wape nchi watashiba ?

Tohara zao ubaya, na nyembe zenye unasaba,
Haya ukijiuzia, mahaba yako msiba,
Kila mjua tumbua, utumbuzi si janaba,
Huo wote hautoshi, wape nchi watashiba ?

Tartila sikujua, na ngazi za ukuruba,
Malimati yakiliwa, huliwa kwenye ujuba,
Na malezi machelewa, heri wasio na baba,
Huo wote hautoshi, wape nchi watashiba ?

No comments: