Thursday, November 8, 2012

Tumeshaondoka GB

TEKNOHAMA neema, wengi wasioijua,


Nyuma wanaangalia, wanashindwa kusogea,

Hofu imewaingia, kuenea teknolojia,

Tumeshaondoka GB, sasa tunakwenda PB !



Ni ujinga au ujuha, mimi siwezi kujua,

Ni sanaa imekuwa, ukuu bila kujua,

Na tunakoelekea, itageuzwa hadaa,

Tumeshaondoka GB, sasa tunakwenda PB !



Chini tumeng'ang'ania, hatutaki kwenda paa,

Anga zimefunguliwa, mitoni tunaogea?

Twashikilia dagaa, papa tunawaachia?

Tumeshaondoka GB, sasa tunakwenda PB !



Vijana kutoandaa, dhuluma ninahofia,

Mengi yangelitufaa, tungeanza wachochea,

Kuunda wakaingia, yale tusiyodhania,

Tumeshaondoka GB, sasa tunakwenda PB !



Laiti ningelikuwa, jopo ningejiundia,

Kwenye kila tasnia, malengo kujiwekea,

Jinsi ya kuitumia, itufae teknolojia,

Tumeshaondoka GB, sasa tunakwenda PB !



Ila wapo wenye njaa, yao wanajifanyia,

Na uadui kuuzua, udugu unapotakiwa,

Wao wamedhamiria, ndio wa kwanza wakawa,

Tumeshaondoka GB, sasa tunakwenda PB !



Tovuti twaiambaa, kando kando kpitia,

Naweza kukuhesabia, wizara zinazojua,

Nyingi sana zafubaa, si kushoto si kulia,

Tumeshaondoka GB, sasa tunakwenda PB !



Matokeo nasikia, uoza wananunua,

Vyenyewe vinavyochaa, pasina ya kutumiwa,

Yakishapita masaa, vipuli hutoopoa,

Tumeshaondoka GB, sasa tunakwenda PB !



Watani nawatania, japo kikongwe najua,

Njia zangu zimejaa, najua pakupitia,

Dunia kujionea, mengine kuwa mzaha,

Tumeshaondoka GB, sasa tunakwenda PB !



Gigabaiti napaa, terra daraja likawa,

Na sasa ninaingia, picabaiti kuvaa,

Inshallah nikijaliwa, nje naenda chukua,

Tumeshaondoka GB, sasa tunakwenda PB !



Inshallah nikijaliwa, nje naenda chukua,

Masomoni nikitua, Asia kusalimia,

Terrabaiti kutwaa, maajabu kujionea,

Tumeshaondoka GB, sasa tunakwenda PB !



Kinyonga tumeshakua, kobe wanatuzidia,

Polepole twatembea, konokono katuoa,

Mme nyuma twafatia, twaenda pasi hatua,

Tumeshaondoka GB, nyie bado mwachelewa ?



Maofisi yatakiwa, kwa fujo kuitimua,

Vijana kuajiriwa, vyuo inaokokotoa,

Maarifa kuenea, nchi tukainyanyua,

Tumeshaondoka GB, nyie bado mwachelewa ?



Majeshi yanatakiwa, vitengo kuvifungua,

Vitu tukavigundua, hata eropleni pia,

Tweze jiendeshea, ofisini tumekaa,

Tumeshaondoka GB, nyie bado mwachelewa ?



Shuleni inatakiwa, kwa wingi iwe yajaa,

Kama bilauri kuwa, hata chini yajimwaiya,

Ustadi ukakua, vyuoni wakiingia,

Tumeshaondoka GB, nyie bado mwachelewa ?



Vijijini yatakiwa, kawi tukifyatua,

Jua inayotumia, au taka nazo pia,

Rahisi sana ikawa, na gharama kupungua,

Tumeshaondoka GB, nyie bado mwachelewa ?



Viongozi watakiwa, tena sana kuijua,

Vihiyo ninaojua, wa kompyuta wakiwa,

Dhamana waliopewa, na bado waikimbia,

Tumeshaondoka GB, nyie bado mwachelewa ?



Kisha nitanukia, Petabaiti kwingia,

Kichochoro nakijua, eksabaiti kutua,

Kisha nikasalimia, zetabaiti jamaa,

Tumeshaondoka GB, sasa tunakwenda PB !



Zetabaiti najua, siwezi kuifikia,

Naona itachelewa, Yotabaiti kungojea,

Kisha brontobaiti, wajukuu kumjua,

Tumeshaondoka GB, sasa tunakwenda PB !



Taifa la kusinzia, kazi huko kufikia,

Mdebwedo watembea, na usiku waingia,

Uso tukija kunawa, mchana imeshakuwa,

Inshallah nikijaliwa, nje naenda chukua,

Tumeshaondoka GB, sasa tunakwenda PB !



No comments: