Friday, November 2, 2012
Kazi ndio imeanza
Kazi ndio imeanza, kujenga demokrasia,
Katiba twatengeneza, ubosi kuuchukua,
Rais tukiamua, pasiwe wa kuzuia,
Mbegu ninawaachia, kupanda mnatakiwa !
Hayawezi wapendeza, utamuni walokaa,
Ajinzi wataifanza, nyufa zipate bakia,
Ili yao kuyatunza, na vya watu kuvitwaa,
Mbegu ninawaachia, kupanda mnatakiwa !
Katiba bila mwangaza, ovyoovyo itakua,
Madudu ikayatunza, watu yasiyosadia,
Hivyo jambo la kufanza, kwanza ni kuielewa,
Mbegu ninawaachia, kupanda mnatakiwa !
Kwanza ni kuyawaza, yakufaa, yasofaa,
Kisha tukabayabwagiza, udhia yanayotia,
Na safi tukayatunza, kizazi kuja kifaa,
Mbegu ninawaachia, kupanda mnatakiwa !
Moja la kuliangaza, rais safi akawa,
Kila kitu kutengeza, na waovu kuwatoa,
Nchi hii kuongoza, raia wanayeridhia,
Mbegu ninawaachia, kupanda mnatakiwa !
Fedha wanaosambaza, mapema kuwagundua,
Na wao kuwabamiza, mbali kutokufikia,
Nchi mwenye kuiweza, fedha kutoabudia,
Mbegu ninawaachia, kupanda mnatakiwa !
Ardhi kutoiuza, jengine kuangalia,
Watu wasije chuuzwa, masikini kubakia,
Hili ninalihimiza, kiranja kusimamia,
Mbegu ninawaachia, kupanda mnatakiwa !
Kulipiga vita giza, hima ninaitoa,
Hatuwezi kuongoza, gizani huku twakaa,
Mwangaza kuueneza, vijijini kusambaa,
Mbegu ninawaachia, kupanda mnatakiwa !
Maji uhai wa kwanza, hili linatangulia,
Kuleta asiyeweza, kitini kumuondoa,
Ifanzike miujiza, yatiririke Tanzania,
Mbegu ninawaachia, kupanda mnatakiwa !
Afya watu kutokwaza, budi bure kutoa,
Kile tunachoingiza, migodini kutumiwa,
Hili kwenu naagiza, sera ninawaachia,
Mbegu ninawaachia, kupanda mnatakiwa !
Elimu nayo kutunza, muhimu bure kutoa,
Kusawazisha yaweza, umma wote Tanzania,
Na kila anayeweza, fedha kikwazo kutokuwa,
Mbegu ninawaachia, kupanda mnatakiwa !
Maliasili kutunza, vizazi ikawafaa,
Na vyanzo kuendeleza, uhai kutochezewa,
Maisha kutochuuza, mengine ni kukataa,
Mbegu ninawaachia, kupanda mnatakiwa !
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment