Friday, November 2, 2012

Kofi la Mungu lauma

UKIKIZIBWA kibao, hakika hukisikia,

Kofi lisilo na ngao, huwezi kulizuia,

Pigo lake ni chaguo, kwenda likiazimia,

Kofi la Mungu lauma, hasa kama waliona !

Kwa Obama ni mwambado, juzi lilikochagua,

Kuna mayowe na kilio, ijapa wasidiwa,

Na onyo walijuao, mapema waliambia,

Kofi la Mungu lauma, hasa kama waliona !

Nawaza kwa siku hiyo, habari pasipokuwa,

Na watu ni walalao, 'singizini wajifia,

Tsunami si mwenzao, huruma itasikia?

Kofi la Mungu lauma, hasa kama waliona !

Al Gore mtukwao, haya aliwaambia,

Taasisi iko mbio, elimu imeshagawa,

Watu wapiga miayo, hawataki kuyajua,

Kofi la Mungu lauma, hasa kama waliona !

Sio tu wao kwao, hata na sisi pia,

Sio tusikiayo, haya tunayoambiwa,

Mazingira tuchafuao, wenyewe tunajiua,

Kofi la Mungu lauma, hasa kama waliona !

Halinao mwelekeo, kofi la Mungu nazaa,

Mbaki meno msagao, radhi likishawamwagia,

Na hakuna tegemeo, mwenyewe anabakia,

Kofi la Mungu lauma, hasa kama waliona !

Bure tujizuzuao, ya Mola kuyachezea,

Kesha kaa mkao, zawadi kutugawia,

Na sisi si tujuao, hadi yanapotokea,

Kofi la Mungu lauma, hasa kama waliona !

Ya kwetu matamania, kitanzi yaije kuwa,

Jalia uwe ni ngao, ya kufaa kuamua,

Tusitafute kilio, kwa ukubwa kujitia,

Kofi la Mungu lauma, hasa kama waliona !

No comments: