Sunday, November 18, 2012

Fukara wa uongozi


Ni mkubwa masikini, akosaye uongozi,

Huishia taabani, asipate usingizi,

Raha awe haioni, nyumbani na matembezi,

Fukara wa uongozi, ni mkubwa masikini !



Ukiipanga thamani, kwanza upe uongozi,

Huu ukiwa makini, zote utapanda ngazi,

Dhaifu ukiauni, mazingira huyawezi,

Fukara wa uongozi, ni mkubwa masikini !



Huchahia akilini, pasiwe na mageuzi,

Wenyewe ukajihini, kwa kuukosa uwazi,

Chenga ukaziamini, magoli ni upandizi,

Fukara wa uongozi, ni mkubwa masikini !



Huathirika moyoni, hauwezi maamuzi,

Uliokuwa laini, kwa hariri vitambazi,

Na msingi huuini, kuja kufanza majenzi,

Fukara wa uongozi, ni mkubwa masikini !



Mipango hujizaini, ikawa na utatizi,

Mikakati kutahini, ikawa ni kubwa kazi,

Rasilimali kuhini, ni ajizi si ujuzi,

Fukara wa uongozi, ni mkubwa masikini !



Inapokufa imani, hukuambaa mwenyezi,

Akakuacha uwani, barazani kubarizi,

Ulicho nacho kichwani, tena kisiwe azizi,

Fukara wa uongozi, ni mkubwa masikini !



Atakaye jiamini, aloweza haliwezi,

Ajitiaye imani, anajua uongozi,

Hufulia hadharani, mafichoni ajienzi,

Fukara wa uongozi, ni mkubwa masikini !



Niepushie Manani, mimi kwako si mjuzi,

Pasina yako ilani, kazi hii siiwezi,

Niongoze mashakani, kivulini nibarizi,

Fukara wa uongozi, ni mkubwa masikini !



No comments: