Wednesday, November 14, 2012

MAJI YAKIZIDI UNGA




Uwakilishi nchini, uwe watu thelathinini,

Mkoa kuwadhamini, wasijeuzwa sokoni,

Tukawa nayo yakini, wanafanza kitu gani,

Maji yakizidi unga, huwa uji si ugali !



China kwenye bilioni, hawazidi ishirini,

Na wote mkutanoni, elfu mbili naamini,

Sisi tuna zuri gani, idadi kuisaini ?

Maji yakizidi unga, huwa uji si ugali !



Rasilimali ni duni, twajitia umaskini,

Kwa kujitia uzani, bila ya hiyo thamani,

Huu ni utundu gani, atwepushe Maanani,

Maji yakizidi unga, huwa uji si ugali !



Twatumia bilioni, na njaa wafa nchini?

Kwayo twamkoga nani, viumbe nawaulizeni ?

Au awapeni nani, vya bure kuviamini?

Maji yakizidi unga, huwa uji si ugali !



Mia tisa takribani, hesabu kuisaini,

Na wote mkutanoni, mia tisa kubaini,

Watachagua makini, kero pasiwepo ndani,

Maji yakizidi unga, huwa uji si ugali !



Zama gani ulizeni, hizi tulizo njiani,

Na nini wanatamani, waliokuwapo chini,

Si fahari na uhuni, ila ya kesho yakini,

Maji yakizidi unga, huwa uji si ugali !



Waenda sema nini, na simu zi mdomoni,

Wanajua kitu gani, tuendako hawaoni,

Hao wamzuga nani, kilivhozidi kichwani,

Maji yakizidi unga, huwa uji si ugali !



Sijaiona yakini, ya kuongeza thamani,

Ila usanii ndani, na nyimbo za uzaini,

Hakuna matumaini, kila mtu yu shakani,

Maji yakizidi unga, huwa uji si ugali !



Wapasao kilingeni, wajue wasema nini,

Kisha kujiulizani, wanamwakilisha nani,

Wametumwa kitu gani, ili wapate auni,

Maji yakizidi unga, huwa uji si ugali !



Nyimbo za utusani, zamsaidia nani,

Kama sio uhuni, na kujishusha thamani,

Mambo sasa umakini, sio ya vijiweni,

Maji yakizidi unga, huwa uji si ugali !



Hivi mna hoja gani, za kutenda jambo gani,

Uishe umaskini, sisi tuwe kivulini,

Maji yaje vijijini, tuoge kwetu uani,

Maji yakizidi unga, huwa uji si ugali !



Mifereji tubaini, tupande kwetu jirani,

Si kwetu mafichoni, pasibaki mtu nyumbani,

Zinatuisha hisani, mgoni hatubaini,

Maji yakizidi unga, huwa uji si ugali !



Twataka tuwe nuruni, si hadhithi viwanjani,

Kasoro hatubaini, umeme kutuzaini,

Toka mwaka wa sitini, karne ya zamani ?

Maji yakizidi unga, huwa uji si ugali !



Haya maendeleo gani, ya kutembea kijani,

Ukiangalia chini, kwa hapo hauioni,

Zinawaka mijengoni, sio kwetu vijijini,

Maji yakizidi unga, huwa uji si ugali !



Watumishi vijijini, tuwekeni ujirani,

Tuwaongeze thamani, kuamke vijijini,

Twawapa umaskini, kisha wamwongoze nani ?

Maji yakizidi unga, huwa uji si ugali !



Mikakati tubaini, wanaofanya auni,

Hao ndio wawe ndani, kati yao thelathini,

Kusimulia kundini, mbinu walizobaini,

Maji yakizidi unga, huwa uji si ugali !



Kusimulia kundini, mbinu walizobaini,

Hata kwao kijijini, kukawa kunashaini,

Tunasaga kina nani, vigelegele kughani ?

Maji yakizidi unga, huwa uji si ugali !



Wawe ni watu makini, wanajenga vijijini,

Maisha kuwa yamini, kuliko kwetu mijini,

Na sisi tukatamani, kurudia vijijini,

Maji yakizidi unga, huwa uji si ugali !



Kwalo ninaamini, chama wengi kitawini,

Kukishakuwa mwangani, huko kwetu vijijini,

Atabisha mtu gani, ustawi hauoni ?

Maji yakizidi unga, huwa uji si ugali !



1 comment:

Unknown said...

Ni wangapi wajuao, malenga namna hizi,
Ni wangapi wasomao, tungo zako tungo hizi,
Ni wangapi wajuao, una tungo kama hizi,
Laiti wangelijuwa, wangezifaidi tungo.

Hongera kwa moyo huo, kuzijaza king'amuzi,
Kazana bila ya tuo,kuzijaza simulizi,
Mimi taweka chapuo, mpaka wazimaizi,
Wasojua watajuwa, waje kufaidi tungo.