Thursday, November 8, 2012

ITAWAKUSANYA





Kuikunja haijawa, mfukoni kuitia,

Mida imeamuliwa, saa zinajipaua,

Mkono waandaliwa, wa Mungu uliokuwa,

Hamtokusanya dunia, ila itawakusanya !



Yaja yasotarajiwa, watu wasioyajua,

Milango ikafungua, darini iliyokuwa,

Pepo wakaachiliwa, duniani kutembea,

Hamtokusanya dunia, ila itawakusanya !



Udi wanafukuzia, na harufu twasikia,

Machoni wasiokuwa, dua wanatuombea,

Malaika washangaa, viumbe kuwaigizia,

Hamtokusanya dunia, ila itawakusanya !



Innahu yakidunaa, wa akidu kaidaa,

Wote wanaitikia, na ndivyo itavyokuwa,

Hakuna linalokuwa, ila Mola kuridhia,

Hamtokusanya dunia, ila itawakusanya !



Yajikusanya dunia, nyaraze kujikusanyia,

Mahemani zikatiwa, au pepo kuchukua,

Yake yalipoanzia, ndiko kule kusokuwa,

Hamtokusanya dunia, ila itawakusanya !



Kitu wala haikuwa, na jambo likazaliwa,

Neno lilipotimia, njia iliandaliwa,

Wengi wetu kupotea, wachache njia kujua,

Hamtokusanya dunia, ila itawakusanya !



Yenu siwezi yajua, hali yangu sijajua,

Ila ninazingatia, niliyoishaamriwa,

Kisha nikayaambaa, yote nisiyoruhusiwa,

Hamtokusanya dunia, ila itawakusanya !



Dunia naihofia, karibu kukaribia,

Mbali mimi nimekaa, siku yangu kungojea,

Na juu nikiingia, pembeni kujikalia,

Hamtokusanya dunia, ila itawakusanya !



No comments: